1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Shirika la HRW: Askari wa Msumbiji wamewaua watoto 10

25 Novemba 2024

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema leo kuwa vikosi vya usalama vya Msumbiji viliwaua watoto 10 na kuwajeruhi wengine 36 katika ghasia za baada ya uchaguzi.

https://p.dw.com/p/4nOKA
Ghasia za baada ya uchaguzi nchini Msumbiji
Ghasia za baada ya uchaguzi nchini Msumbiji.Picha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Human Rights Watch imeongeza kuwa polisi imewakamata "mamia ya watoto bila ya kuzijulisha familia zao, hatua ambayo ni kinyume na sheria za kimataifa za haki za binadamu."

Hata hivyo, mamlaka haijajibu ripoti hiyo iliyotolewa na Human Rights Watch.

Nchi hiyo ya kusini mwa Afrika imekumbwa na ghasia tangu uchaguzi wa Oktoba 9 ulioshindwa na chama tawala cha Frelimo ambacho kimekuwa madarakani tangu uhuru, ingawa matokeo hayo yamepingwa na upinzani.

Maelfu ya watu wameandamana kote nchini katika wiki za hivi karibuni, japo maandamano hayo yamekabiliwa vikali na polisi.

Rais Filipe Nyusi ambaye anatarajiwa kuondoka madarakani mnamo mwezi Januari, amelaani kile alichokiita "jaribio la kuchochea machafuko” katika hotuba ya hali ya taifa aliyoitoa wiki iliyopita.