Gavi kununua chanjo 500,000 za Mpox kwa ajili ya Afrika
18 Septemba 2024Kundi la ufadhili wa chanjo ulimwenguni, Gavi, limesema kuwa litanunua dozi 500,000 za Mpox kutoka kampuni ya Bavarian Nordic kwa ajili ya kusaidia kupambana na mripuko wa ugonjwa wa homa ya nyani barani Afrika.
Shirika hilo ambalo hufadhili ununuzi wa chanjo kwa nchi za kipato cha chini, limesema kuwa litatumia kiasi cha dola milioni 50 katika mpango huo, unaojumuisha usafirishaji, usambazaji na gharama za usimamizi wa chanjo.
Soma: Ugonjwa wa mpox watangazwa kuwa dharura ya afya ya umma
Chanjo hizo zitatolewa mwaka huu. Takribani dozi milioni 3.6 za Mpox tayari zimeahidiwa kutolewa na mataifa tajiri duniani kwa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, lakini hadi sasa ni kiasi kidogo tu ambacho kimewasili.
Kumeripotiwa visa 25,000 vya ugonjwa wa Mpox na vifo 723 barani Afrika, zaidi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO.