310713 Mali Wahlen
31 Julai 2013Wafuasi wa Keita wanashangilia huku matokeo kamili ya mwisho yakikaribia kutolewa. Kwao ni shangwe na nderemo. Wanasema mchezo umekwisha. Mgombea wao ameshashinda na atakuwa rais mpya wa Mali.
Waziri wa mambo ya ndani wa Mali, Kanali Moussa Sinko Coulibaly, alitangaza jana kwamba Keita amewaacha mbali wapinzani wake na kama hali hiyo itaendelea ina maana hakutakuwa na haja ya kufanyika duru ya pili ya uchaguzi. Matokeo hayo yalitangazwa baada ya theluthi moja ya kura zote kuhesabiwa.
Wafuasi wa upinzani wameghadhabishwa sana na tangazo hilo. Inna Maiga ni mfuasi wa waziri wa zamani wa fedha wa Mali, Soumaila Cisse, anayeshikilia nafasi ya pili kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyotangazwa. "Hatukubaliani kabisa na kilichofanyika; Waziri kutangaza matokeo! Tumemtaka ataje asilimai ya takwimu lakini hakufanya hivyo. Bila kusema uongo, hatua hiyo inaweza kuibua matatizo.
Mshindi wa uchaguzi ni Mali
Licha ya mjadala unaoendelea kuhusu takwimu, asilimia ya kura na uwezekano wa kufanyika duru ya pili ya uchaguzi, tayari kuna mshindi katika uchaguzi huo -naye ni taifa la Mali. Hii ni kwa sababu uchaguzi ulifanyika vizuri kuliko ilivyotarajiwa. Kulikuwa na hofu waasi wangefanya mashambulio ya kigaidi, lakini kulikuwa shwari. Na ndio maana uchaguzi huo umepongezwa sana, hata na Richard Zink, Mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya mjini Bamako.
"Ushiriki katika uchaguzi huu pekee ni ufanisi mkubwa sana na pia jinsi ulivyofanyika. Nadhani wanachotaka kukisema Wamali kiko wazi. Wanasema, Tunataka kubeba mustakabali wa nchi yetu mikononi mwetu na tunataka mwanzo mpya."
Hata changamoto za maandalizi hazikusababisha matatizo makubwa sana kiasi cha kuathiri zoezi la upigaji kura.
Busara itumike katika kutangaza matokeo
Kutangaza haraka matokeo ya uchaguzi huo, kunaweza kusababisha balaa, ameonya Christopher Fomunyoh, Mkurugenzi wa taasi ya kitaifa ya Demokrasia kwa ajili ya masuala ya kimataifa, NDI, barani Afrika. "Nadhani wanachojali raia wa Mali ni uwazi wa mchakato mzima. Ukionekana kuwa wazi, halali na wa haki, Wamali watayakubali matokeo bila kujali yatakavyokuwa. Lakini kukiwa na hisia kuna mtu aliyeziendea kinyume sheria ili atangazwe mshindi, tutashuhudia watu wakipaza sauti kulalamika.
Uchaguzi wa Jumapili ulikuwa muhimu kwa mustakabali wa Mali. Ni wa kwanza tangu mapinduzi ya kijeshi ya Machi 22 mwaka uliopita, yaliyofuatiwa na miezi kadhaa ya kukaliwa eneo la kaskazini na waasi wa Vuguvugu la kitaifa kwa ukombozi wa taifa la Azawad, MNLA, na ni hatua muhimu kuelekea demokrasia.
Mwanajeshi wa Ufaransa afariki
Huku hayo yakiendelea mwanajeshi mmoja wa Ufaransa amekufa na mwingine kujeruhiwa kwenye ajali ya barabarani kaskazini mwa Mali. Kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya ulinzi, ajali hiyo imetokea wakati gari alimokuwa akisafiria lilipoanguka na kuingia kwenye mtaro. Mwanajeshi huyo, Marc Martin-Valler, mwenye umri wa miaka 28, ni wa saba kufa tangu Ufaransa ilipoanza operesheni yake nchini Mali Januari 11 mwaka huu.
Mwandishi: Josephat Charo/Gänsler Katrin
Mhariri: Yusuf Saumu