Boubakar Keita adai ushindi Mali
30 Julai 2013Kundi linalohusika na kampeini ya mgombea urais Ibrahim Boubacar Keita,aliyekuwa waziri mkuu nchini Mali linasema kwa mujibu wa matokeo wanayoyafahamu wao yanamuweka mgombea wao katika nafasi ya mbele kwa kura nyingi kabisa na hapana shaka atashinda uchaguzi huo wa duru ya mwanzo kwa kishindo.
Lakini kauli hiyo haikubaliki kabisa na wapinzani,wanasema wanahakika duru ya pili itahitajika.Taarifa hizo za pande zote mbili zimekuja katika wakati ambapo matokeo rasmi yanasubiriwa na kwa maana hiyo wengi wanahisi hiyo ni ishara ya mwanzo ya kutokea mivutano baada ya uchaguzi huo wa Jumapili uliofanyika salama.
Kwa upande mwingine kutoshuhudiwa ghasia hadi wakati huu na kujitokeza kwa idadi kubwa ya wapiga kura kunatafsiriwa na wengi kwamba ni hatua inayoonyesha ni kwa kiasi gani wananchi wa Mali walivyo na hamu kubwa ya kuanza ukurasa mpya wa maisha baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa vurugu,mivutano na vita pamoja na mapinduzi ya kijeshi.Wapinzani wa Keita,ambao ni pamoja na aliyekuwa waziri wa fedha Soumali Cisse,Modibo Sidibe,aliyekuwa waziri mkuu na Dramane Dembele ambaye ni mgombea wa chama kikubwa kabisa nchini Mali kwa pamoja wanasema wanaamini kwa vyovyote vile itahitajika duru ya pili.
Wote watatu ni wanachama wa muungano wa FDR,ulioundwa kupambana na utawala wa kijeshi mwaka jana.Cisse ambaye anaonekana kuwa ni mpinzani mkubwa wa Keita amesema atayapinga matokeo mahakamani ikiwa duru ya pili haitoitishwa.Mgombea huyo anadai udanganyifu wa kupangwa na mizengwe ilishuhudiwa takriban katika mji mzima wa Bamako.Hata hivyo chama cha MNLA kinachopigania kujitenga kwa taifa la AZAWAD na ambacho hakikushiriki katika uchaguzi huo kimesema kiko tayari kushirikiana na yoyote atakayetangazwa mshindi katika uchaguzi huo.
Matokeo kamili ya uchaguzi huo huenda yakatangazwa siku ya Ijumaa (02.08.2013) na ikiwa italazimika kufanyika duru ya pili kwa maana kwamba hakuna atakayefanikiwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura basi itabidi duru hiyo ifanyike Agosti 11.Itakumbukwa kwamba Umoja wa Mataifa umewatolea mwito wagombea wote kuheshimu matokeo ya uchaguzi hata ikiwa zoezi hilo lilikuwa na dosari.
Mwandishi:Saumu Mwasimba/Reuters/Afp
Mhariri:Mohammed AbdulRahman