Shambulio la kujitoa muhanga lauwa 15 Yemen
30 Januari 2018Kulingana na wakaazi, watu waliyojihami kwa bunduki walianza kukimiminia risasi kituo hicho cha ukaguzi baada ya mshambuliaji wa kujitolea muhanga kuendesha gari lililosheheni mabomu katika kituo hicho Kaskazini Mashariki mwa mji wa Ataq katika jimbo la Shabwa. Maafisa wamesema watu 15 wameuwawa katika shambulizi hilo huku watu watatu wakijeruhiwa.
Shambulizi hili limetokea wakati jeshi linalotaka kujitenga Kusini mwa Yemen likipambana na vikosi vya serikali huku pande zote zikiwania kuudhibiti mji wa Aden mji ulio na serikali ya mpito ya rais Abd-Rabbu Mansour Hadi.
Mapigano hayo yalikuwa katika hatari ya mapigano mengine tofauti ya kampeni inayoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran Kaskazini mwa nchi hiyo.
Hata hivyo hakuna kundi lolote llililojitokeza kukiri kuhusika na mashambulizi ya leo asubuhi.
Lakini mashambulizi haya yanasemekana kufanana na operesheni za awali zinazofanywa na kundi la kigaidi la Al Qaeda katika rasi ya kiarabu linaloendesha shughuli zake katika eneo hilo.
Aidha kikosi cha Shabwa , kilichoundwa na kupewa mafunzo na Umoja wa falme za kiarabu kwa lengo la kupambana na wanamgambo wa kiislamu liliwatoa wapiganaji wa Al Qaeda nje ya mji wa Ataq katika operesheni kubwa ya kijeshi mwezi Agosti mwaka jana.
Muungano wa kampeni ya kijeshi inayoongozwa na Saudi Arabia unasema una nia ya kuikomboa Yemen
UAE ni miongoni mwa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia uliyoiingialia kati vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen mwaka 2015 kujaribu kumrejesha rais Hadi madarakani baada ya waasi wa Houthi kujiimarisha mjini Aden. Msemaji wa muungano wa kampeni ya kijeshi inayoongozwa na Saudi Arabia Turki al-Maliki, amesema bado wanaendelea na azma yao ya kuikomboa Yemen.
Tangu mwaka wa 2014 Yemen imekuwa katika mgogoro waa kugombea madaraka kati ya rais anayetambuliwa kimataifa Abdu Rabu Mansour Hadi na waasi wa kihouthi wanaoungwa mkono na Iran. Mwezi Machi mwaka 2015 Saudi Arabia na washirika wake kisuni walianzisha mashambulizi ya angani dhidi ya kundi la Washia wakati lilipoanza kujiimarisha mjini Aden.
Wakati huo huo maafisa wa usalama nchini Yemen wanasema Waziri Mkuu Ahmed Obaid Bin Daghar anajitayarisha kuitoroka nchi hiyo baada ya jeshi linalotaka kujitenga kushikilia jengo la rais kusini mwa mji wa bandari wa Aden katika mapigano makali yaliyodumu usiku wa kuamkia leo.
Maafisa hao wamesema wapiganaji waliyotiifu kwa baraza la mpito walipigana hadi katika jengo la rais la Maashiq. Mapigano mjini Aden yalizuka upya siku ya jumapili wakati tarehe ya mwisho iliyotokewa na jeshi linalotaka kujitenga kutaka serikali ijiuzulu kumalizika.
Rais Hadi hata hivyo ameitaja hatua ya jeshi hilo kuwa jaribio la mapinduzi.
Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/dpa/AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman