1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shalit awasili Israel, Wapalestina wawapokea mashujaa wao

18 Oktoba 2011

Hatimaye Gilad Shalit amewasili nyumbani Israel kuungana na familia yake baada ya siku 1,941 mikononi mwa Hamas, kupitia mabadilishano ya wafungwa ambayo yameshuhudia Wapalestina 477 wakiachiliwa kutoka jela za Israel.

https://p.dw.com/p/12uVN
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu (kushoto), akimkaribisha Gilad Shalit.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu (kushoto), akimkaribisha Gilad Shalit.Picha: dapd

Kwenye mji wa Mitzpe Hila, kaskazini mwa Israel, ambako ndiko kwao Shalit, nderemo na vifijo vilitawala wakati picha za Shalit zilipooneshwa kwenye televisheni kwa mara ya kwanza. Shamrashamra hizo zilizidi maradufu baada ya kuwasili nyumbani kwao.

Mapema kabla ya kuondoka Misri mchana wa leo kurudi kwao, Shalit alikiambia kituo cha televisheni cha Nile cha Misri, kwamba alikuwa ana shauku sana ya kuwoana watu wake.

Shauku ilikuwa pia kwa kundi la Hamas ambalo limefanikisha mpango mkubwa kuwahi kutokea kwenye historia ya Mashariki ya Kati - kuachiliwa huru Wapalestina 477 kwa mkupuo mmoja hivi leo na wengine 550 wanafuatia.

Aziza Qawasmi, mama wa Kipalestina ambaye mtoto wake ni miongoni mwa wafungwa walioachiwa leo, ameonekana akilia kwa furaha katika viwanja vya Rafah.

"Hii ni siku ya furaha kwa Waislamu na watu wetu wote. Nataraji watu wote watakuwa na furaha kama yangu kwa sababu wafungwa hawa ni watoto wetu. Hii ni sikukuu kwetu kukutana na watoto wetu." Amesema Aziza.

Mmoja wa wafungwa wa Kipalestina akionesha alama ya V, kuashiria uhuru, karibu na kuachiwa na Israel.
Mmoja wa wafungwa wa Kipalestina akionesha alama ya V, kuashiria uhuru, karibu na kuachiwa na Israel.Picha: dapd

Lakini kwa upande wa viongozi wa kisiasa kutoka pande zote, hili ni tukio lenye malengo zaidi ya kubadilishana wafungwa tu. Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ameliita tukio zima kama gumu lakini muhimu sana, si kwa Shalit peke yake, bali kwa amani ya Israel nzima. Hata hivyo, amesisitiza kuwa Israel itaendelea kupambana na wale anaowaita magaidi.

Hamas kwa upande wao, wamesema kwamba huu si mwisho, bali bado kuna mengi ya kufanywa, likiwemo Israel kuuondolea vikwazo Ukanda wa Gaza.

Akiwa Rafah kwenye mpaka wa Misri, Makamo Mwenyekiti wa Hamas, Mussa Abu Marzuk.

"Israel inapaswa kufahamu kuwa inalazimika kuwaachilia huru wafungwa waliobakia. Ikiwa haitawaachia katika mazingira ya kawaida, watawaachia katika mazingira mengine." Amesema Marzuk.

Kwenye Ukingo wa Magharibi, mjini Ramallah, ambako wafungwa 117 walipokelewa kishujaa, Rais wa Mamlaka ya ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas, aliwaambia maelfu ya Wapalestina waliokusanyika kwenye mapokezi hayo, kwamba kujitolea kwao, juhudi yao, na kazi ngumu waliyoifanya, haikuangukia patupu.

Katika jumuiya ya kimataifa, Katibu Mkuu ya Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameuita ubadilishanaji huu wa wafungwa kama hatua moja mbele katika kuelekea amani kati ya Israel na Palestina.

Mfuasi wa Hamas akifurahia mpango wa kubadilishana wafungwa kati ya Israel na Palestina.
Mfuasi wa Hamas akifurahia mpango wa kubadilishana wafungwa kati ya Israel na Palestina.Picha: dapd

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, aliye hivi sasa ziarani nchini Libya amepongeza kuachiwa kwa Shalit na kuongeza kuwa anatarajia Mmarekani uraia pia Israel, Ilan Grapel, naye ataachiliwa huru kutoka jela ya Misri.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, William Hague, amekiita kitendo hiki kuwa ni cha ujasiri, lakini akaitaka Israel ijitolee zaidi kutafuta amani na Wapalsetina.

"Tunaamini Israel inapaswa kuwa tayari kufanya maamuzi magumu zaidi ya vile viongozi wake walivyoonesha hadi sasa." Amesema Hague akiwa jijini London.

Naye Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa, ameliita tukio hili kama faraja kwa nchi yake, akiongeza kwamba sasa mazungumzo ya amani yanatakiwa yaanze mara moja.

Shalit ana uraia wa Israel na Ufaransa na Rais Sarkozy amesema anaamini kuwa, ukweli huu ndio uliomfanya awe hai mpaka leo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo