Israel na Hamas wakubaliana kubadilishana wafungwa
12 Oktoba 2011Tangu wakati huo Gilad Shalit amekuwa akishikiliwa kizuwizini. Serikali ya Israel na Hamas wamekuwa kila wakati wakifanya mazungumzo ya jinsi ya kubadilishana Shalit na wafungwa wa kipalastina. Usiku wa kuamkia leo, jumatano, makubaliano yameweza kufikiwa. Baada ya kikao cha dharura kilichodumu takriban saa tano, mawaziri wa serikali ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu wameunga mkono kwa wingi makubaliano hayo.
"Gilad atarejea nyumbani kwa familia yake na wananchi wenzake mnao siku zijazo. Kama wasemavyo waliotutangulia wenye busara: Yeyote anaeokoa roho, anauokoa ulimwengu mzima". Leo usiku nimependekeza serikalini namna ya kumuokoa Gilad Shalit, ili hatimae, na baada ya miaka mitano, apate kuokolewa na kurejea nyumbani Israel."
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametangaza habari hizo za kubadilishana wafungwa huku akikunja uso.Familia za wahanga wa mashambulio ya wapalastina daima wamekuwa wakilalamika kwamba waliowauwa jamaa zao sasa wataachiwa huru.
Hata hivyo, baraza la mawaziri limeunga mkono mpango wa kubadilishana wafungwa katika kikao kilichofanyika jana usiku. Mawaziri 26 wameunga mkono pendekezo hilo, watatu wamepinga, miongoni mwao akiwemo waziri wa mambo ya nchi za nje mfuasi wa siasa kali za kizalendo, Avigdor Liebermann. Kabla ya hapo, ujumbe wa Israel ulikubaliana na wawakilishi wa Hamas kuachiliwa huru Gilad Shalit kwende sambamba na kuachiliwa huru zaidi ya wafungwa elfu moja wa kipalastina. Katika awamu ya mwanzo wafungwa 450 wataachiwa huru. 280 kati yao wamehukumiwa kifungo cha maisha.
Mkuu wa idara ya upelelezi ya Israel, Yoram Cohen, aliwaelezea kwa kina zaidi mawaziri mpango huo wa kubadilishana wafungwa. Mpango huo unazungumzia juu ya kurejeshwa wafungwa 110 wa kipalastina katika maeneo walikotokea ya Ukingo wa magharibi na Jerusalem ya mashariki. Wafungwa 131 wakaazi wa Gaza watarejeshwa pia Gaza. Wapalastina 203 wa ukingo wa magharibi hawatoruhusiwa kurejea nyumbani, badala yake watapelekwa Gaza au nchi za nje. Waisrael sita wenye asili ya kiarabu nao pia wataachiwa huru.
Zaidi ya hayo, Israel imeahidi kuwaachia huru katika kipindi cha miezi miwili ijayo, wafungwa 550 watakaosalia. Maafisa wasiopungua watatu wa ngazi ya juu wa Hamas kutoka ukingo wa magharibi hawataachiwa huru-amesema mkuu wa idara ya upelelezi ya Israel-Yoram Cohen. Wanahusika na mashambulio yaliyogharimu maisha ya raia wa kiisrael. Hata Marwan Barghouti, mmojawapo wa viongozi mashuhuri wa chama cha Fatah, kwa mujibu wa duru za habari za Israel, hatoachiwa huru.
Watakaoachiwa huru watakabiliana na hatua kali: nusu ya wafungwa watakaorejea ukingo wa magharibi hawatakuwa na ruhusa ya kulihama eneo hilo na baadhi bao hawatakuwa hata na ruhusa ya kutoka mji mmoja kwenda katika mji mwengine.
Noam Shalit, babaake mwanajeshi Gilad Shalit amesema baada ya kikao cha baraza la mawaziri,mwanawe ataachiliwa huru baada ya kupitisha miaka mitano,siku 1935 bila ya kulifumba jicho.
Mwandishi:Engelbrecht Sebastian/Tel Aviv(BR)/Hamidou Oummilkheir
Mhariri : Miraji Othman