Serikali ya Umoja wa Kitaifa Afghanistan leo
21 Septemba 2014Yumkini Ashraf Ghani ambaye kulingana na matokeo ya awali aliishinda duru ya pili ya uchaguzi atatangazwa kuwa rais, huku mpinzani wake Abdullah Abdullah akiachiwa jukumu la kumteuwa mtu katika wadhifa mpya ulioundwa, ''Afisa Mkuu wa Utawala'', kukiwa na uwezekano wa yeye mwenyewe kujiweka katika nafasi hiyo. Kila mmoja wa wagombea hao, Ghani na Abdullah, anadai alishinda duru ya pili ya uchaguzi.
Vile vile, matokeo ya mwisho baada ya kura za duru ya pili ya uchaguzi kuhesabiwa upya yanatarajiwa kuwekwa hadharani. Hayo yamethibitishwa na msemaji wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Afghanistan, Noor Mohammed Noor, hapo jana.
Kutangazwa kwa matokeo hayo kuliahirishwa kwenye dakika ya mwisho, kutoa nafasi kwa mazungumzo yaliyolenga kumaliza utata ambao ulikuwa ukitishia kuizamisha Afghanistan katika mgogoro mkubwa, huku vikosi vya kimataifa vinavyoongozwa na Marekani vikijiandaa kuondoka katika nchi hiyo.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa
Aimal Faizi ambaye ni msemaji wa rais Hamid Karzai anayemaliza muda wake, amesema kupitia ukurasa wake wa Twitter hapo jana, kwamba ''Wagombea wote wawili wanatazamiwa kutia saini makubaliano juu ya muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Jumapili''.
Katika ya Afghanistan inampa rais madaraka makubwa, na serikali mpya ya nchi hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa itokanayo na kuzorota kwa sekta muhimu za uchumi na usalama. Mchakato wa kuhesabu kura ulikumbwa na matatizo mengi huku kukiwa na madai kuwa zoezi zima lilizongwa na mizengwe, hali ambayo inaliimarisha kundi la Taliban, na kuudhoofisha zaidi uchumi wa nchi hiyo ambao bado unategemea msaada kutoka nje.
Utata kuhusu uhusiano na NATO
Mustakabali wa uhusiano baina ya Afghanistan na Umoja wa Kujihami wa NATO ni suala jingine lenye utata, kwa sababu Karzai amekaidi kutia saini makubaliano ya kiulinzi, ambayo yangeruhusu kuendelea kuwepo kwa wanajeshi wa kigeni kwenye ardhi ya Afghanistan baada ya ujumbe rasmi wa kijeshi wa umoja huo kumalizika rasmi mwaka huu.
Maafisa wakuu wa NATO wameelezea matumaini kuwa kuundwa kwa serikali ya kitaifa kutaharakisha kutiwa saini kwa makubaliano hayo yaliyokwama. Jenerali Philip Breedlove kutoka Marekani ambaye ndiye kamanda mkuu wa vikosi vya NATO nchini Afghanistan, amesema makubaliano hayo ni muhimu yafikiwe kabla ya kuanza mchakato mwingine wa kuzungumzia jinsi umoja huo utakavyoendelea kuisaidia Afghanistan.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/RTRE
Mhariri:Bruce Amani