1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa uchaguzi waendelea Afghanistan

Josephat Nyiro Charo27 Agosti 2014

Zoezi la kuhakiki kura linaendelea licha ya wagombea wawili kujiondoa leo (27.08.2014). Mchakato huo unalenga kusuluhisha mzozo wa uchaguzi ulioibuka kufuatia duru ya pili ya uchaguzi Juni 14 mwaka huu.

https://p.dw.com/p/1D2hZ
PT Präsidentschaftskandidaten für die Wahlen in Afghanistan 2014
Abdullah Abdullah, kushoto, na Ashraf Ghani, kuliaPicha: Getty Images

Mkwamo umezidi leo nchini Afghanistan kuhusiana na matokeo ya uchaguzi wa urais baada ya wagombea wote wawili wanaotaka kumrithi rais wa sasa Hamid Karzai, kuwaondoa waangalizi wao kutoka kwa mchakato wa kuhakiki kura unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa. Mchakato huo unaolenga kusuluhisha mzozo wa uchaguzi ulioibuka kufuatia duru ya pili ya uchaguzi mnamo mwezi Juni mwaka huu, unaendelea.

Zoezi la kuhakiki kura lilikuwa sehemu ya makubaliano yaliyosimamiwa na Marekani kutuliza wasiwasi na mvutano uliokuwa ukizidi kati ya mahasimu wawili Abdullah Abdullah na Ashraf Ghani, ambao wote wamedai kushinda uchaguzi ulionuiwa kuashiria hatua ya kwanza ya kidemokrasia ya kukabidhi madaraka.

"Tumejiondoa kutoka kwenye mchakato leo kwa sababu hauna maana kwetu. Acha waendelee," amesema Fazel Ahmad Manawi, mhakiki mkuu wa Abdullah, alipozungumza na shirika la habari la Reuters mapema leo.

Saa chache baadaye, Umoja wa Mataifa umeitaka timu ya Ghani pia iwaondoe waangalizi wake kwa masilahi ya haki, kwa mujibu wa mwanachama wa timu ya waangalizi wa Ghani, Daoud Sultanzoy. Sultanzoy amesema ingawa inaonekana si haki kuachana na zoezi hilo, kisiasa inaonekana kuwa uamuzi wa uadilifu.

Afghanistan Präsidentschaftswahl Kandidat Abdullah Abdullah Archiv 11.06.21014
Abdullah AbdullahPicha: Wakil Kohsar/AFP/Getty Images

Awali Fazel Ahmad Manawi, ambaye ni mkaguzi mkuu wa mgombea Abdulla Abdullah alionya kuhusu mchakato huo wa kuhakiki kura. "Kama masharti yetu hayatatimizwa, kama Umoja wa Mataifa au tume ya uchaguzi au timu ya Ghani itaendelea na mchakato huu, hilo litakuwa jukumu lao na sio letu." Manawi ameongeza kusema, "Na matokeo yoyote yatakayofuata, hatutakuwa na dhamana."

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, John Kerry amefanya ziara mbili Afghanistan tangu Juni 14 kutuliza hali ya mambo na kuwashinikiza mahasimu hao wakubaliane kushirikiana. Maafisa wa Marekani waliingilia kati tena siku ya Jumatano (26.08.2014) na kufanya mazungumzo ya dharura na Abdullah, kwa mujibu wa mwanachama wa timu yake ya waangalizi katika mchakato wa kuhakiki kura.

Zoezi linaendelea

Umoja wa Mataifa ulikuwa umethibitisha mchakato huo ulikuwa umetatizwa kwa muda. Maafisa wa umoja huo na tume huru ya uchaguzi ya Afghanistan wamethibitisha zoezi hilo linaendelea bila waangalizi wa pande zote mbili kuwepo na maafisa wanaohusishwa katika kazi hiyo wanasema huenda Ghani hatimaye akathibitishwa kuwa rais.

Tume ya uchaguzi inasema watu milioni 8.1 walipiga kura katika duru ya pili ya uchaguzi wa urais mnamo Juni 14 mwaka huu, lakini Abdullah anakataa takwimu hizo, akidai wapigaji kura waliojitokeza ni wachache na kura zisizo halali zilitumbukizwa kwa njia ya udanganyifu kwenye masunduku ya kupigia kura na mpinzani wake.

Afghanistan Stimmen werden neu ausgezählt 27.08.2014
Kura zaendelea kuhesabiwa upyaPicha: Reuters

Abdullah amesema atayakataa matokeo ya mwisho ya uchaguzi baada ya zoezi kukamilika kwa mujibu wa msemaji wake, Muslim Saadat, katika taarifa aliyoitolea leo baada ya kujiondoa.

Wasiwasi wazidi Afghanistan

Mzozo kuhusu kura umezidisha wasiwasi wa kukosekana uthabiti, kuwepo machafuko na hata pengine kuanza awamu mpya ya mapigano katika taifa hilo linalopambana na uasi wa kundi la wanamgambo wa Taliban. Hii leo vikosi vya Afghanistan vimekabiliana na wapiganaji wa Taliban kutaka kulidhibiti jimbo la kaskazini la Kunduz, huku wanamgambo hao wakitishia kuuteka mji mkuu wa jimbo hilo na kuwahangaisha wakaazi waliokimbilia wilaya jirani.

Kamanda wa jeshi la polisi katika wilaya ya Chahar Darah, Abdul Shukor Surki, amesema watu wana wasiwasi na wengi tayari wamekimbilia maeneo salama nje ya Kunduz.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/AFPE

Mhariri: Iddi Ismail Ssessanga