1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sera ya ujenzi wa makazi ya walowezi yalaaniwa vikali

Sylvia Mwehozi
19 Novemba 2019

Syria, Misri, Jordan na Umoja wa Mataifa, zimelaani tangazo la Marekani la kwamba haizingatii tena ujenzi wa makazi ya walowezi unaofanywa na Israel kuwa unakiuka sheria za kimataifa.

https://p.dw.com/p/3TJPl
Israel | Siedlungsbau
Picha: imago images/UPI Photo

Katika taarifa iliyotolewa na shirika la habari la Syria SANA, chanzo kimoja katika wizara ya mambo ya nje, kimesema Damascus, "inalaani vikali msimamo wa Marekani kuelekea sera ya ujenzi wa makazi ya walowezi katika maeneo ya Wapalestina, ambayo ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa".

Taarifa hiyo imeongeza kwamba Syria inautizama msimamo wa Marekani kuwa "batili na usio na athari za kisheria". Misri nayo imesema kwamba inafuata maazimio ya kimataifa na sheria, zinazozingatia ujenzi huo kuwa "haramu na unaokiuka sheria za kimataifa, kulingana na msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Ahmed Hafez.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Jordan Ayman al-Safadi alielezea ujenzi huo wa makazi ya walowezi kuwa "ni hatua zisizo kubalika" na kwamba zinadhoofisha nafasi ya kupatikana suluhisho la mataifa mawili. Al-Safadi alionya juu ya "athari" zitakazojitokeza katika mchakato wa amani kutokana na uamuzi wa Marekani.

Palästina Israel | Konflikte | Nethanjahu genehmigt vor Wahl israelische Siedlung von Mevoot Jericho im Westjordanland
Kibao kinachoonya Israel kuingia maeneo ya WapalestinaPicha: Getty Images/A. Levy

Nayo ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, ilithibitisha msimamo wake kwamba ujenzi wa makazi ya walowezi katika maeneo ya Wapalestina ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa, na hivyo inakataa msimamo mpya wa utawala wa Marekani kuelekea sera ya ujenzi. Msemaji wa ofisi hiyo Rupert Colville amesema " mabadiliko katika msimamo wa sera wa taifa moja hakubadili sheria za kimataifa zilizopo wala tafsiri yake katika mahakama ya kimataifa ya haki na Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa". Mpatanishi mkuu wa Palestina kwenye mazungumzo ya amani Saeb Erekat ameutaja uamuzi wa Marekani kuwa batili.

"Kauli ya waziri Pompeo kadri tunavyofahamu ni batili. Ni kujiondoa kwa utawala wa Trump katika ulingo wa sheria za kimataifa. Na pindi unapojiondoa katika ulingo huo, basi unafungua milango ya machafuko, ugaidi, misimamo mikali na rushwa", alisema Erekat.

Uturuki ni nchi nyingine ambayo imelaani tangazo hilo. Waziri wake wa mambo ya nje Mevlut Cavusuglo aliandika katika ukurasa wa twitter kwamba maamuzi kama hayo hayatakuwa na uhalali wowote katika sheria za kimataifa, akiongeza kwamba hakuna nchi iliyo juu ya sheria hizo. Uturuki ambayo ni mtetezi thabiti wa Palestina pia ilikosoa uamuzi wa Marekani kuutambua mji wa Jerusalemkama mji mkuu wa Isreal mwaka 2017.