1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yasema ubalozi mpya mjini Jerusalem ni Historia

14 Mei 2018

Marekani imeufungua rasmi ubalozi wake mpya katika mji wa Jerusalem huku Wapalestina zaidi ya 40 wakiuwawa na mamia wengine wakijeruhiwa kwenye mapambano na askari wa Israel katika harakati za kuipinga hatua hiyo.

https://p.dw.com/p/2xhmI
Israel Eröffnung der US-Botschaft in Jerusalem | Videobotschaft von Donald Trump
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Scheiner

Hatua ya Marekani ya kuuhamishia rasmi ubalozi wake kwenye mji  wa Jerusalem kutoka Tel Aviv imetekelezwa baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuitambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel.

Balozi wa Marekani nchini Israel David Friedman amesema kuwa baada ya miaka 70 ya kuanzishwa kwa taifa la Israel wakati muhimu kama huu na wa kihistoria ni kwa sababu ya ujasiri wa mtu mmoja tu ambaye ni rais wa Marekani Donald Trump. Rais huyo wa Marekani hakuhudhuria sherehe hizo lakini alitoa hotuba kupitia kwenye Video.

Trump amesema Marekani itaendelea kujitolea kikamilifu katika kuuwezesha mpango wa amani wa Mashariki ya Kati. Jared Kushner mkwe wa Trump na mke wake Ivanka binti yake Trump ambao ni wasaidizi wa rais huyo, waliuongoza ujumbe wa Marekani kwenye sherehe hizo.

Balozi wa Marekani nchini Israel David Friedman
Balozi wa Marekani nchini Israel David FriedmanPicha: Reuters/R. Zvulun

Wakati sherehe hizo zilipokuwa zikifanyika Wapalestina waliendelea kufanya maandamano makubwa kwenye mpaka wa Gaza na Israeli. Kwa furaha kubwa tele waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amemsifu rais Trump na kumshukuru kwa kuileta historia hii.

Hatua ya kuhamishwa ubalozi wa Marekani nchini Israel kutoka mjini Tel Aviv na kuupeleka katika mji wa Jerusalem imewachukiza mno Wapalestina, ambao wanataka mji wa Jerusalem mashariki kuwa mji mkuu wa taifa la baadae la Palestina. Wizara ya Afya katika Ukanda wa Gaza imetangaza kuwa zaidi ya Wapalestina 40 wameuawa huku wengine zaidi ya 1900 wakiwa wamejeruhiwa.

Ubalozi huo wa Marekani umefunguliwa mjini Jerusalem wakati amabpo Wapalestina wanaomboleza siku ya maafa ya Al-Naqba yaani siku ya kuundwa kwa taifa la Israel miaka 70 iliyopita tarehe 15 Mei.

Wakati huo huo serikali ya Ujerumani imeelezea wasi wasi wake juu ya mgogoro wa Mashariki ya Kati. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani amesema kufunguliwa kwa ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem kusiwe sababu ya kufanya ghasia. Msemaji huyo pia ameeleza kuwa Israel nayo inapaswa kuzingatia kanuni ya kujizuia. Katika tamko hilo Ujerumani imesema ina uhakika kwamba suluhisho juu ya suala la Jerusalem linaweza kupatikana kwa njia ya mazungumzo.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas Picha: picture-alliance/AA/C. Karadag

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini ametoa mwito kuzitaka pande zote zijizuie na amesisitiza juu ya umuhimu wa suluhisho la nchi mbili baina ya Israel na Palestina.

Ufaransa pia imetoa mwito kwa pande zote kujizuia ili kupunguza maafa. Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa amesema haungi mkono hatua ya Marekani. Waziri mkuu wa Palestina Rami Hamdallah amesema uamuzi wa Marekani wa kuitambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel unakiuka sheria za kimataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres naye ameelezea wasi wasi wake juu ya idadi ya watu waliouawa karibu na mpaka baina ya Ukanda wa Gaza na Israel. Wakati huo huo Umoja wa nchi za Kiarabu unatarajiwa kuitisha kikao cha dharura ili kujadili uamuzi wa Marekani. Naibu katibu mkuu wa umoja huo, Saeed Abu Ali, ameeleza kwamba wajumbe kwenye mkutano wa Jumatano, huko mjini Cairo watajadili njia za kuukabili uamuzi huo.

Wizara ya mambo ya nje ya Uturuki imesema aamuzi wa Marekani kuhamishia ubalozi wake hadi mjini Jerusalem ulihamasisha vikosi vya Israeli kuwaua waandamanaji wa Kipalestina kwenye mpaka wa Gaza na kwamba Uturuki inalaani mauaji hayo yaliyofanywa na maafisa wa usalama wa Israeli.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/RTRE/DPA

Mhariri: Iddi Ssessanga