1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Seneta wa upinzani Kongo Ponyo amshtaki spika wa Seneti

Jean Noël Ba-Mweze
22 Juni 2023

Seneta wa upinzani nchini Kongo Augustin Matata Ponyo ambae pia ni Waziri Mkuu wa zamani, ameondoa imani yake kwenye ofisi ya Seneti na kumshtaki Spika wa Seneti hiyo, Modeste Bahati Lukwebo, mbele ya mahakama kuu

https://p.dw.com/p/4SxH4
DR Kongo Ex-Premierminister Augustin Matata Ponyo
Picha: Florida Zantoto/Press Office Primeminister Kongo

Seneta wa upinzani nchini Kongo Augustin Matata Ponyo ambae pia ni Waziri Mkuu wa zamani, ameondoa imani yake kwenye ofisi ya Seneti na kumshtaki Spika wa Seneti hiyo, Modeste Bahati Lukwebo, mbele ya mahakma kuu jana Jumatano,  baada ya Lukwebo kukubali ombi jipya la mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya katiba ili kumuondolea tena kinga ya ubunge na hivyo kuanza upya kesi inayomkabili. Upande wake Matata amekosoa njia zinazotumika zikilenga  kumuondoa kwenye kinyang'anyiro cha kugombea  urais kwani tayari ameshatangaza kujitosa kwenye kinyang'anyiro hicho.

Akishutumiwa kwa ubadhirifu wa fedha zilizokusudiwa kuboresha bustani ya kilimo ya Bukangalonzo, Matata Ponyo alifunguliwa kesi mwezi Mei 2021 katika Mahakama ya Kikatiba. Lakini mnamo Novemba mwaka huo huo, Mahakama hayo ikajitangaza kuwa haina uwezo wa kumhukumu waziri mkuu wa zamani.

Soma pia: Seneta Matata Ponyo adai kupewa sumu nchini Congo

Martin Fayulu zu Besuch bei der DW in Bonn
Mgombea wa urais Fayulu alijiondoa akidai udanganyifuPicha: Dirke Köpp/DW

Swali hilo liliibuka tena wiki iliyopita wakati mwendesha mashtaka mkuu kwenye Mahakama ya Kikatiba alipowasilisha ombi jipya kwenyi ofisi ya Seneti ili kuruhusiwa mara nyingine kumshtaki Seneta Matata akisisitiza kuwa tayari ushahidi mwengine umeongezeka kuhusu swali la Bukangalonzo na lile la ubadhirifu wa fedha zilizokusudiwa kuwalipa wahanga wa zairianization, yaani siasa iliyotumiwa na utawala wa raïs wa zamani Joseph-Desiré Mobutu ili kupokonya mali za wageni. Halafu Spika Modeste Bahati Lukwebo akakubali ombi hilo kupitia matamshi haya:

"Tunaamini kuwa kwa hatua hii hatuna budi kuamua tena kwa mara ya pili, kwani mwenzetu bado yupo mikononi mwa vyombo vya sheria. Ni lazima mahakama kuendelea kuichunguza kesi hiyo kwani kwetu sisi bado hajarudishiwa kinga zake."

Hayo yanajiri miezi sita kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hapa nyumbani. Seneta Matata Ponyo ambaye pia ni kiongozi wa chama cha LGD ni mmoja wa wagombea ambao tayari wametangaza kuwania urais dhidi ya Félix Tshisekedi.

Matata Ponyo anakosoa kile anachokitaja kuwa ujanja unaolenga kumweka kando akiamini kuwa hatua za kisheria zinazofanywa dhidi yake na Mwendesha Mashtaka mkuu kwa ushirikiano na ofisi ya Seneti sizo halali kwani Spika wa Seneti ni mmoja wa viongozi wa muungano wa vyama vinavyomuunga mkono Rais Félix Tshisekedi, ndivyo alivyoeleza Matata Ponyo baada ya kumshtaki Bahati Lukwebo mbele ya mahakama kuu.

"Tangu leo naondoa imani yangu yote kwa Spika wa Seneti na ofisi yake. Hii ni mara ya kwanza haya kutokea hapa nchini. Nimewasilisha mashtaka mbele ya mahakma kuu dhidi ya Spika Modeste Bahati Lukwebo kwani  amekiuka Katiba na kanuni zetu za ndani, akishirikiana na mwendesha mashtaka mkuu ili kufanya vitendo ambavyo havikubaliki."

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaandaa kufanya chaguzi nne mnamo Disemba 20, ambazo ni uchaguzi wa rais, ule wa wabunge wa taifa na wa mikoa, pamoja na chaguzi za manispaa. Lakini wapinzani Joseph Kabila na Martin Fayulu tayari wamejiondoa wakisema mchakato unajaa na udanganyifu.