1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Seneta Matata Ponyo adai kupewa sumu nchini Congo

Saleh Mwanamilongo
20 Julai 2021

Waziri Mkuu wa zamani wa Congo, Matata Ponyo amedai kupewa sumu wakati uchunguzi wa mahakama ukiendelea katika mashtaka yanayomkabili ya ubadhirifu wa fedha.

https://p.dw.com/p/3wjVy
Waziri Mkuu wa zamani wa Congo (2012-2016), Matata Ponyo adai kupewa sumu
Waziri Mkuu wa zamani wa Congo (2012-2016), Matata Ponyo adai kupewa sumuPicha: Florida Zantoto/Press Office Primeminister Kongo

Matata Ponyo ambaye DW imewasiliana naye muda mfupi uliopita amesema hawezi kuzungumza hivi sasa  kutokana na maumivu mwilini. Kwenye mtandao wake wa twitter,hii leo, Matata amesema amepewa sumu na kuwataka wananchi wa Congo kumuombea apate nafuu. Matata Ponyo amesema uchunguzi wa mwanzo wa madaktari umebaini kwamba alipewa sumu. Lakini haijulikani lini na katika mazingira gani waziri Mkuu huyo wa zamani alinyweshwa sumu.

''Ameandamwa kwa njia nyingine,hata kupewa sumu''

Mawakili wa Matata wameomba kuweko na uchunguzi ili kubaini namna sumu hiyo ilivyoingia mwilini mwake. Stefane Kamundala , wakili na mkuu wa asasi za kiraia jimboni Maniema amesema nilazima hatua kali ichukuliwe kwa atakayebainika kupanga au kuratibu jambo hilo.

 ''Tunasikitika na kuanza kuwa na woga kwamba kesho au baada ya kesho huduma ya matibabu yake yasiwe nzuri, na kufikia kumpoteza mwanasiasa wa ngazi yake. Tumeshuhudia pia,ikiwa hawawezi kumfungulia mtu mashtaka kisheria, ameandamwa kwa njia nyingine hata kwa kupewa sumu ili atoweke.''

Njama za kisiasa ?

Matata amekanusha tuhuma zote dhidi yake na kusema ni njama ya kisiasa
Matata amekanusha tuhuma zote dhidi yake na kusema ni njama ya kisiasaPicha: DW/S. Mwanamilongo

Kabla ya tangazo hilo kutolewa Matata alitakiwa kujiripoti leo kwenye ofisi ya mwendesha mashtaka wa korti kuu ya taifa. Juhudi za DW za kupata maelezo ya ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu vwa taifa kuhusu madai hayo ya Matata Ponyo hazikufua dafu.  Msemaji wa serikali ya Congo ameimbia DW kwamba hawezi kuzungumzia maswala ya kisheria.

Wiki liopita Matata aliwekewa kifungo cha nyumbani kabla ya uamzi huo kubatilishwa na mahakama. Matata amekabiliwa wa mashataka ya ubadhirifu wa fedha wakati alipokuwa Waziri Mkuu.

Mnamo mwezi Mei waendesha mashtaka waliomba bunge kumwondolea kinga waziri mkuu huyo wa zamani Matata Ponyo ambaye sasa ni seneta ili aweze kuchunguzwa kuhusiana na madai ya ufisadi lakini bunge la senet lilipiga kura ya kupinga ombi hilo kwa sababu mahakama ya katiba nchini humo iliyotoa ombi hilo haina mamlaka ya kuwafungulia mashtaka wabunge. Matata amekuwa akikanusha tuhuma zote dhidi yake na kusema ni njama ya kutaka kumyamazisha kisiasa.