1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sehemu ya kura kuhesabiwa tena Georgia

29 Oktoba 2024

Tume kuu ya uchaguzi nchini Georgia imesema kura zitahesabiwa tena kwenye asilimia 14 ya vituo vya kupigia kura baada ya wachunguzi huru kuibua wasiwasi kuhusu mwenendo wa uchaguzi wa wabunge wa siku ya Jumamosi.

https://p.dw.com/p/4mMfv
Georgia
Sehemu ya kura kuhesabiwa tena GeorgiaPicha: Irakli Gedenidze/REUTERS

Kulingana na matokeo rasmi, chama tawala cha Georgian Dream kilishinda kwa kupata karibu asilimia 54 ya kura, lakini wawakilishi wa vyama vya upinzani vinavyoegemea upande wa Magharibi pamoja na rais wa Georgia wamesema matokeo hayo yalichakachuliwa.

Maelfu ya watu waandamana Georgia kupinga uchaguzi wa bunge

Maelfu ya watu wameandamana katika mji mkuu, Tbilisi, kupinga matokeo hayo. Umoja wa Ulaya, Jumuiya ya Kujihami ya NATO pamoja na  Marekani zimetaka kufanyike uchunguzi kamili juu ya madai ya wapiga kura kununuliwa, kufanyika vitisho na kujazwa kura bandia katika masunduku ya kupigia kura.

Tume ya uchaguzi ambayo hapo awali ilitangaza kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki imesema sehemu ya kura zitahesabiwa tena, lakini haikusema ni lini matokeo yatatolewa hadharani.