Scholz ataka ushindani sawa biashara ya magari na China
15 Aprili 2024Scholz ambaye yuko ziarani nchini China amesema magari ya China yatapewa nafasi katika soko la Ujerumani lakini akaonya kuhusu utumiaji wa mbinu zisizo za haki za kibiashara.
Ujerumani inafaidika na bidhaa kutokana na mahitaji ya bidhaa kutoka China kuanzia magari hadi kemikali lakini mahusiano ya nchi hizo mbili yanayumba kufuatia kampuni za Ujerumani kusema zinakumbana na vizingiti visivyo vya haki katika biashara zao nchini China.
Kansela huyo wa Ujerumani anamalizia ziara yake ya siku tatu nchini China hii leo, aliyoandamana na ujumbe mkubwa wa wafanya biashara na wakurugenzi kadhaa wa kampuni za kijerumani. Katika ziara yake hiyo Scholz pia aliizungumzia Taiwan bila ya kuitaja moja kwa moja akiitahadharisha China kwamba kuionea nchi ndogo ni makosa.