Ethiopia na Eritrea zaanza safari ya mahusiano mema
18 Julai 2018Shirika la ndege la Ethiopia, liliweka picha ya ndege yake yenye nambari za safari ET0312 katika mtandao wake wa kijamii wa twitter, ikiondoka mjini Addis Ababa kuelekea mji Mkuu wa Eritrea Asmara.
Miongoni mwa waliokuwemo katika ndege hiyo ni watu waliokuwa na hamu ya kuungana na familia zao baada ya kutenganishwa na mgogoro huo wa muda mrefu.
Aliekuwa waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, pia alikuwepo katika ndege hiyo.
Kulingana na mwandishi habari wa shirika la AFP aliyeabiri ndege hiyo, kinywaji aina ya champagne kilitolewa kwa abiria wote waliogongeshana glasi muda mfupi baada ya ndege hiyo kuondoka.
Vile vile wahudumu wa ndege waliokuwa wakitabasamu waliwakabidhi abiria wote maua.
Shirika la ndege la Ethiopia moja ya mashirika ya ndege yanayokuwa kwa haraka barani Afrika limesema litakuwa na ndege moja kila siku ya kwenda na kurudi kutoka addis Ababa hadi Asmara nchini Eritrea.
Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Tewolde GebreMariam, ameongeza kuwa huenda wakaongeza safari hizo hadi mara mbili au mara tatu kwa siku kutokana na wingi wa abiria.
Mahusiano mapya ya Ethiopia na Eritrea yanatarajiwa kupiga jeki uchumi wa nchi hizo.
Siku ya Jumatatu rais wa Eritrea Isaias Afwerki alifungua tena ubalozi wa Eritrea mjini Addis Ababa. Kurejesha mahusiano yaliovunjika kwa muda mrefu baina ya Ethiopia na Eritrea kunatarajiwa kupiga jeki uchumi wa nchi hizo mbili. Wakati huo huo shirika la Amnesty International limesema amani mpya iliyopatikana inapaswa kuwa nafasi mpya ya mabadiliko kwa Eritrea moja ya mataifa yaliotengwa duniani.
Juhudi za kidiplomasia za kuleta amani kati ya mataifa hayo mawili zilianza mwezi uliopita wakati mpenda mabadiliko Waziri Mkuu mpya wa Ethiopia Abiy Ahmed aliye na miaka 42, allipoukubali mpango wa amani uliomaliza vita vya mpakani vilivyoanzia mwaka 1998 hadi mwaka 2000.
Baada ya hapo viongozi wa Ethiopia na Eritrea walianza mara moja kutembeleana na kukaribishana kwa kukumbatiana. Jamii ya Kimataifa kwa upande wake imakaribisha na kusifu kumalizika kwa moja ya migogoro ya muda mrefu barani Afrika.
Mawasiliano ya simu yamerejeshwa na mahusiano ya kiuchumi yameanza kurejeshwa huku Ethiopia nchi isiokuwa na bandari ikiwa na nia ya kujiendeleza kupitia bandari ya Eritrea ya eneo la bahari nyekundu.
Mwandishi: Amina Abubakar AP/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga