SADC imesitisha mkutano wake kufuatia hofu ya Corona
10 Machi 2020Hatua hiyo imefikiwa baada ya mawaziri wananoshughulikia sekta ya Afya katika jumuia hiyo kuketi kwa dharura hapo jana na kujadili hali halisi ya COVID-19 duniani na katika nchi wananchama na maandalizi ndani ya jumuia katika kukabiliana na virusi hivyo pamoja na hatua za kuchukuliwa kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.
Virusi vya Corona tayari umekwisha shambulia takriban mataifa 101 ulimwenguni kati ya mataifa 194.
Sehemu ya makubaliano ya mawaziri wa afya ni kuzuia mikutano ambayo inaweza kuzuilika hivyo kuafiki mkutano wa baraza la mawaziri wa fedha, mipango, viwanda, biashara na mambo ya nje kufanyika kwa njia ya video ambapo kila mshiriki atakuwa nchini mwake wakati mkutano ukiendelea.
Akitoa taarifa ya kubadilishwa kwa mfumo huo wa mkutano katibu mkuu wizara ya mambo ya nje nchini Tanzania balozi kanali Wilbert Ibughe amesema utaratibu huo wa kuendesha mkutano kwa njia ya video umeridhiwa na sekretarieti ya SADC pamoja na nchi mwenyekiti kwa kuwa unalenga kuondoa hatari ya kuenea kwa ugonjwa endapo mmoja kati ya washiriki atakuwa amepata maambukizi.
"Sasa kufuatia ushauri uliotolewa katika maazimio ya kikao cha mawaziri wa afya wa SADC jana, kikao cha baraza la mawaziri wa SADC kilichokuwa kimepangwa kimefupishwa na sasa kitaafanyika kwa njia ya video tarehe 18," alisema balozi kanali Wilbert Ibughe.
Tanzania imezitaka serikali za SADC kuchukua hatua zinazopendekezwa na wataalamu wa afya ili kujikinga na Corona
Ikumbukwe kuwa utaratibu huu wa kufanya mkutano kwa njia ya video kwa jumuia hiyo utakuwa ni wa kwanza kufanyika ambapo Tanzania kama mwenyekiti imezitaka serikali za SADC kuchukua hatua stahiki zinazopendekezwa na wataalamu wa afya ili kujikinga na ugonjwa huo hatari ambao tayari nchi mwananchama wa SADC Afrika kusini imethibitisha kuwepo kwa wagonjwa takriban saba.
Naibu katibu mkuu mtendaji anaeshughulikia utengamano wa SADC dokta Tembikosi Mpongo amewaambia wanahabari kuwa kama jumuia inafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanalinda afya za wakaazi ikiwemo kuepuka mikusanyiko inayohatarisha kuenea kwa ugonjwa huo.
"Kipaumbele cha kwanza cha serikali ni kuwakinga watu wake na hivyo tunafanya kwa kuzuia makutano ya aina kwa ana yasio ya lazima ambapo maambukizi yanaweza kutokea, hii si kwetu tu ni ulimwegu mzima umechukua hatua kama hii ili inapotokea hatua za haraka zinachukuliwa kukabiliana lakini kwanza ni kudhibiti kadri inavyowezekana," alisema dokta Tembikosi Mpongo
Tangu kuzuka kwa Virusi vya COVID-19 ama Corona mwishoni mwa mwaka uliopita tayari vimeshaua zaidi ya 3,100 nchini china, 463 Italia na barani Afrika, Misri imeripoti kifo cha kwanza kutokana na ugonjwa huo na nchi kadhaa zimethibitisha kupatikana kwa wagonjwa walioambukizwa virusi hivyo ikiwemo Afrika kusini, Nigeria, Algeria pamoja na Senegal.
Chanzo: Hawa Bihoga DW Dar es salaam