1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Rusesabagina aachiwa huru

25 Machi 2023

Paul Rusesabagina aliyekuwa akizuiliwa jela kwa madai ya kuikosoa serikali ya Rwanda ameachiliwa huru jana usiku Marekani imesema, huku ikiishukuru Kigali kwa hatua hiyo.

https://p.dw.com/p/4PERb
Ruanda Paul Rusesabagina
Picha: Cyril Ndegeya/Xinhua/IMAGO

Paul Rusesabaginaraia wa Ubelgiji na mkazi wa kudumu wa Marekani baada ya kuachiliwa alikwenda moja kwa moja hadi kwenye makazi ya balozi wa Qatar mjini Kigali, hii ikiwa ni kulingana na afisa wa Marekani na huenda akabaki kwenye makazi hayo kwa siku kadhaa kabla ya kwenda Qatar, iliyosaidia mchakato wa kuachiliwa kwake.

Soma Zaidi: Mahakama ya Rwanda yamkuta Rusesabagina na hatia ya ugaidi

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken ametoa taarifa ya kukaribisha hatua hiyo ya kuachiliwa kwa Rusesabagina, ingawa maafisa wa Marekani walisema hakukua na ahadi yoyote ambayo wangeitoa kwa Kigali zaidi ya kuitambua tu hatua hiyo hadharani.

Ni faraja kujua kwamba Paul anaungana na familia yake na serikali ya Marekani inaishukuru serikali ya Rwanda kwa kufanikisha kuwaunganisha," alisema Blinken. "Pia tunaishukuru serikali ya Qatar kwa msaada wao muhimu ambao utamwezesha Paul kurejea Marekani."

Filmstill I Kinofilm "Hotel Ruanda"
Sehemu ya filamu ya Hotel Rwanda ambayo ilimpatia umaarufu mkubwa Paul RusesabaginaPicha: Tobis Film/picture-alliance

Rusesabagina, shujaa wa filamu ya Hotel Rwanda aliyesifika kwa kuokoa maisha ya watu 1,200 katika hoteli aliyoisimamia wakati wa mauaji ya kimbari ya 1994 alikua mkosoaji wa rais Paul Kagame na alihukumiwa kifungo cha miaka 25 jela kwa tuhuma za ugaidi.

Katika hotuba iliyoandikwa kwa uangalifu mkubwa, Blinken alikosoa machafuko ya kisiasa, lakini bila ya kuunga mkono madai ya Rwanda dhidi ya Rusesabagina. "Marekani ina imani na Rwanda ambayo ina amani na ustawi," alisema. "Tunatumaini mabadiliko ya kisiasa nchini Rwanda na duniani kote yatapatikana kwa njia za amani. Ghasia za kisiasa hazina nafasi."

Afisa wa Marekani amesema kuachiliwa kwake bado hakujabadilisha wasiwasi wa Marekani kuhusu jukumu la Rwanda mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kulikogubikwa na machafuko yanayochochewa na mashambulizi ya wanamgambo wa M23. Blinken akubaliana na madai kwamba Kigali inawaunga mkono waasi hao.