Riek Machar akimbilia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
19 Agosti 2016Kwa mujibu wa afisa mmoja kutoka chama chake cha SPLM-IO kwasasa Machar yuko mjini Kinshasa na anataka kuondoka haraka iwezekanavyo kwenda Ethiopia.Taarifa iliyotolewa mapema leo na chama cha Machar,ilisema kiongozi huyo alifanikiwa kuhamia taifa jirani,bila kuweka wazi aliko.Hakuna aliyekuwa akifahamu alikotorokea kiongozi huyo wa zamani wa waasi,baada ya kuzuka mapigano mapya kati ya wanajeshi wake na wale wa serikali mwezi Julai mwaka huu.
Wiki kadhaa baada ya kuondoka Juba,rais Salva Kiir alimteua Taban Deng Gai kuchukua nafasi ya Machar ya makamu wa rais wa kwanza. Deng Gai alikuwa rafiki na mshirika wa karibu wa Machar,lakini alikatisha uhusiano nae baada ya kukataa kwenda nae mafichoni baada ya kuzuka mapigano.Wakati wa ziara yake nchini Kenya Deng Gai alimlaumu Machar kwa kuhujumu amani katika taifa hilo changa zaidi duniani.
Hata hiyo alimshauri arejee nyumbani ili kujiandaa kwa uchaguzi mkuu mwaka 2018. “Popote alipo aombe kuruhusiwa kupita bila kutatizwa.Aishi kwa amani taifa lolote atakalochagua,iwe mjini Juba au eneo analotaka.Na kama anahisi hawezi kuishi Juba aje Kenya au taifa lingine barani Afrika, Akipange chama chake cha kisiasa na kusubiri uchaguzi mkuu mwaka 2018” alisema Deng Gai
Hata hivyo Den Gai amesema ataachia madaraka mradi tu Machar arejee mjini Juba. Uamuzi wa Machar kusafiri Ethiopia,taifa ambalo limeshiriki katika kuandaa mazungumzo ya amani Sudan kusini kupitia jumuiya ya ushirikiano wa maendeleo ya nchi za mashariki na pembe ya Afrika IGAD, unadhihirisha hana nia yeyote ya kutojumuishwa katika mazungumzo au kuondolewa madarakani. Makanda kadhaa wa zamani wa kundi la waasi tayari walikuwa wameikosoa hatua ya Deng Gai kuchua nafasi ya makamu wa rais na kusema ni msaliti.
Na katika taarifa nyingine, Umoja wa mataifa umeanzisha uchunguzi kuhusu shambulizi katika hoteli moja Sudan Kusini,amapo wanajeshi wanadaiwa kuwabaka akinamama na kuwashambulia wafanyaikazi kutoka mashirika ya kutoa misaada.
Shambulizi hilo la tarehe 11 mwezi Julai katika hoteli ya Terrain mjini Juba lilitokana na machafuko yaliyokumba mji huo kwa siku nne mwezi uliopita.Ijumaa iliyopita baraza la usalama la umoja wa Mataifa lilidhinisha azimio lilotayarishwa na marekani kuongezwa wanajeshi zaidi elfu 4 kutoka idadi ya sasa ambayo ni elfu 12. Wanajeshi hao kutoka Afrika watakuwa na uwezo wa kukabiliana na wale wanaowatisha raia japo watakuwa chini ya Umoja wa mataifa.
Mwandishi: Jane Nyingi
Mhariri: Iddi Ssessanga