Vikosi vya Kiir na Machar Sudan Kusini kuunganishwa
18 Agosti 2016Upande mmoja unamuunga mkono rais Salva Kiir huku ule mwingine ukimtii Riek Machar. Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Nairobi nchini Kenya Deng Gai amesema hatua hiyo huenda ikaisadia kurejesha utulivu katika taifa hilo changa kabisa duniani.
Kauli hiyo ya Deng Gai inatokana na machafuko ya hivi karibuni nchini Sudan kusini yaliyotokana na makabiliano kati ya wanajeshi wa Rais Kiir na wale watiifu kwa Machar. Hadi sasa haifahamiki wapi aliko Machar ambae alikuwa makamu wa rais wa Kwanza baada ya kuondoka mji mkuu juba kufuatia machafuko hayo yaliyosababisha vifo vya mamia ya watu na maelfu ya wengine kutafuta hifadhi katika mataifa jirani.
Msemaji wa Machar alisema kiongozi wao alilazimika kuondoka na vikosi vyake mjini Juba ili kuepusha mapigano zaidi. Kwa mujibu wa Deng Gai vikosi hivyo viwili vitakuwa vimeunganishwa na kuwa kimoja kufikia mwezi Mei mwaka ujao.
“Vikosi hivyo havina mafunzo ya kutosha na vina miliki silaha nzito na hilo limesababisha hali tunayoishuhudia kwasasa.Tunajitahidi kuzuia kutokea mzozo mwingine kama huu kati ya majeshi ya serikali yale ya upinzani,na ndio maana nasema tunaharakisha kuviunganisha vikosi hivyo viwili na kuwa jeshi moja la jamuhuri ya Sudan Kusini” alisema Deng Gai
Hata hiyo Deng Gai alimyooshea kidole cha lawama Machar kwa mkwamo uliopo kufanikishwa mkataba wa amani Sudan kusini. Makamu huyo wa kwanza wa rais alisema hasa walitofautiana vikali na Machar baada ya kutofuata agizo lake la kumtaka waondoka pamoja Juba mwezi Julai mwaka huu baada ya kutokea machafuko.
Hata hiyo alisisitiza hali sasa ni tulivu Juba “Hakuna mapigano yoyote yanayoendelea Juba, kama yapo machafuko yeyote pengine ni eneo la magharibi katika mpaka kati ya Sudan Kusini na jamuhuri ya kidemokrasi ya Kongo.Kwa hivyo nyie waandishi wa habari mnaoripoti kuhusu Sudan Kusini andikeni taarifa za kweli sisi ni taifa changa na tunahitaji uungwaji mkono kutoka kwa kila mmoja.”
Wakati wa ziara yake nchini Kenya Deng Gai pia alikutana na rais Uhuru Kenyatta kumwarifu hatua walizopiga kufanikisha mkataba wa amani na pia kumwomba msaada wa kuijenga upya Sudan Kusini.Taifa hilo bado linasubiri mkutano wa viongozi wa eneo hilo utakaofanyika mjini Juba kujadili kupelekwa kikosi cha Afrika kitakachokua chini ya Umoja wa Mataifa .Kikosi hicho kitakuwa na uwezo wa kukabiliana na wale watakaowatishia raia.
Mwandishi: Jane Nyingi
Mhariri: Iddi Ssessanga