Ramaphosa asema hakuna nafasi ya vurugu Afrika Kusini
3 Juni 2024Matokeo rasmi yaliyotangazwa siku ya Jumapili (02.06.2024) yalikuwa mabaya kwa chama tawala cha African National Congress ANC, ambacho ni chama kikongwe cha ukombozi barani Afrika kilichowahi kuongozwa na Nelson Mandela, miaka 30 iliyopita na kuondoa utawala wa wazungu.
Wapiga kura waliokasirishwa na kupanda kwa viwango vya ukosefu wa ajira, uchumi kuyumba na kutokuwa unavyohitajika, kutokuwa na usawa pamoja na mgao wa umeme, walikiadhibu chama hicho kwa kutokiunga mkono kikamilifu katika uchaguzi wa bunge na kukipa asilimia 40.2 ya kura, ukilinganisha na uchaguzi wa mwaka 2019 wa bunge, ambapo chama hicho kilijizolea asilimia 57.5 ya kura.
Ramaphosa atoa wito wa ushirikiano Afrika Kusini
Matokeo haya yanamaanisha chama cha ANC hakikupata zaidi ya asilimia 50 ya kura kukifanya kiweze kuunda serikali, kwahivyo ni lazima kigawane madaraka na mpinzani wake mkuu wa kisiasa ili kiendelee kuwepo madarakani. Akizungumza baada ya matokeo hayo kutangazwa, Ramaphosa alisema huu ndio wakati wa kuwa na uongozi uliowajibika, kufanya kazi pamoja na kwamba hakuna nafasi ya vitisho au taifa kutokuwa thabiti katika kipindi hiki alichokiita muhimu kwa viongozi kuungana kwaajili ya taifa na wananchi wake.
"Kile uchaguzi huu ulichotuonesha ni kwamba, watu wa Afrika kusini wanatarajia viongozi wao kufanya kazi pamoja, ili kufanikisha mahitaji yao. Wanatarajia vyama walivyovipigia kura kutafuta njia ya pamoja na kutatua tofauti zao na kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya kila mmoja," Alisema rais Ramaphosa.
ANC ni lazima itafute mshirika wa kuunda serikali ya mseto
Kupungua kwa umaarufu wa chama cha ANC, kumeanzisha minon'gono kwamba huenda siku za Ramaphosa madarakani zinakaribia kukamilika aidha kutokana na washirika watakaokuwepo katika serikali ya mseto, au kutokana na changamoto za uongozi ndani ya chama. Lakini hadi sasa maafisa wote wakuu ndani ya chama hicho, wanamuunga mkono Ramaphosa na wachambuzi wanasema hakuna mrithi wa wazi wa kuchukua nafasi hiyo.
Chama cha ANC chahitaji washirika kuunda serikali ya mseto
Inabidi sasa chama hicho kiungane na chama kimoja au zaidi ya kimoja kuendesha serikali na kumchagua Ramaphosa kama rais kwa muhula wa pili. Uchaguzi Mkuu wa Afrika Kusini unaanza kwa uchaguzi wa Bunge ambao utaamua ni viti vingapi kila chama inachopata bungeni, na baadae wabunge ndio wanaomchagua rais. Kulingana na matokeo yaliyotolewa chama cha ANC kimepata viti 159 kati ya jumla ya viti 400 katika bunge la nchi hiyo, kikifuatiwa na chama cha Democratic Alliance kilichopata viti 87 na uMkhonto weSizwe chake rais wa zamani Jacob Zuma kikipata viti 58.
Huku hayo yakiarifiwa, chama hicho cha uMkhonto we Sizwe kimesema kinafikiria kuyapinga matokeo hayo mahakamani, licha ya kufanya vizuri kuliko wengi walivyotarajia na kuchukua nafasi ya tatu kwa kujizolea asilimia 14.6 ya kura.
reuters,ap,afp