China na Ujerumani zaonya dhidi ya vizuizi vya kibiashara
17 Aprili 2024Viongozi hao wawili walisisitiza haja ya kuepukana na sera za ulinzi wa masoko. Xi alisema uhusiano na Ujerumani utaendelea kukua kama mataifa yote yataheshimiana na kutafuta maelewano.
Soma pia: Mkakati wa Ujerumani wa China wakaribishwa Taiwan, wakosolewa Beijing
Scholz alisema anataka kufanya kazi na uongozi wa China ili kuyaboresha mazingira ya makampuni ya Ujerumani nchini China. Siku ya Jumatatu, Scholz alisema kuwa ushindani kati ya China na Ujerumani unapaswa kuwa wa haki na akaonya Beijing dhidi ya kutekeleza sera za ulinzi wa masoko katika sekta ya magari.
Hii ilikuwa ziara ya kwanza ya Kansela Scholz nchini China tangu Berlin ilipoutangaza mkakati wake wa kibiashara mwaka wa 2023. Mkakati huo unalenga kuhakikisha kuwa Ujerumani haiitegemei sana China, ambayo ndio nchi ya pili kubwa kiuchumi ulimwenguni.