Salva Kiir atoa wito kwa wakimbizi kurejea nyumbani
23 Februari 2023Ombi la rais Salva Kiir limekuja wakati Sudan Kusini ikijiandaa kufanya uchaguzi wake wa kwanza, tangu ilipojipatia uhuru kutoka Sudan mwaka 2011. Uchaguzi uliocheleweshwa nchini humo unatarajiwa kufanyika Desemba mwaka 2024.
Rais Kiir amewahakikishia watu wanaorejea nchini usalama wao, na kutoa wito kwa washirika wa kimataifa kuiunga mkono serikali katika kuwashirikisha tena kwenye jamii.
5 wauawa katika jimbo la Blue Nile nchini Sudan
"Kwa wale watakaoamua kurejea nyumbani katika maeneo yao ya asili, serikali itawahakikishia usalama wao, na wale wasioweza kurejea katika jamii zao watapewa kipande cha ardhi katika majimbo kulioko makambi ya watu waliopoteza makaazi yao,"aliongeza kusema rais Salva Kiir.
Ombi la Kiir linakuja wiki kadhaa baada ya ziara ya Papa Francis
Mkutano wa rais Kiir umefanyika wiki mbili baada ya Papa Francis aliyezuru taifa hilo, kukutana na raia wa Sudan Kusini waliokimbia makazi yao katika mji mkuu, Juba, na kuomba amani ya kudumu.
Taifa hilo changa duniani bado linajaribu kujinasua kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka mitano vilivyoanza mwaka 2013, na kusababisha vifo vya maelfu ya watu na hatimae kumalizika kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotiwa saini mwaka 2018. Kwa muda, raia wa Sudan Kusini waliokimbia waliunda kundi kubwa zaidi la wakimbizi duniani katika nchi jirani ya Uganda.
"Wakati tukiendelea na hatua za kuyafanikisha makubaliano ya amani, na kuandaa uchaguzi mkuu utakaohitimisha kipindi cha mpito, kitakachofuata na tutakachokipa kipaumbele ni warejesha watu wetu kutoka katika makambi yalioko nchi za nje," alisema Kiir.
Chanzo: ap