Rais wa Iran akamilisha ziara yake China
16 Februari 2023Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa na nchi hizo mbili leo Alhamisi, Rais wa China Xi Jinping amekubali kwa furaha mwaliko wa Rais wa Iran Ebrahim Raisi wa kufanya ziara mjini Tehran. Hakuna tarehe rasmi iliyotolewa ya ziara hiyo, ambayo itakuwa ya kwanza kwa Xi katika taifa hilo la Mashariki ya Kati tangu mwaka 2016.
Beijing na Tehran ziliimarisha uhusiano wao mpana wa kiuchumi mnamo mwaka 2021 kwa kutia saini mkataba wa ushirikiano wa kimkakati wa miaka 25 lakini zimekuwa zikikabiliwa na shinikizo kutoka kwa mataifa ya Magharibi juu ya misimamo yao kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Soma zaidi: China, Iran watoa mwito wa kuondolewa vikwazo vya Iran
Iran inakabiliwa pia na vikwazo vikali vya Marekani kutokana na mpango wake wa nyuklia. Jamhuri hiyo ya Kiislam ilikubaliana na mataifa yenye nguvu duniani mwaka 2015 kudhibiti mpango wake wa nyuklia, na kama fidia, ingeondolewa vikwazo.
Lakini Rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump aliiondoa nchi yake katika makubaliano hayo mnamo mwaka 2018 na akaiwekea tena vikwazo, jambo lililopelekea Tehran kutotekeleza ahadi zake.
Juhudi za kufufua makubaliano hayo zimekwama kwa miezi kadhaa, huku Marekani na Israel zikiendelea kuishutumu Iran kuwa ina nia ya kutengeneza silaha za nyuklia, madai ambayo Iran inayakanusha.
China na Iran zatoa wito wa kusitishwa vikwazo
Beijing na Tehran zimetoa wito leo wa kusitishwa kwa vikwazo, zikilaumu hali ya mvutano wa sasa na kusema umesababishwa na kitendo cha Marekani kujiondoa katika makubaliano ya awali.
Katika taarifa ya pamoja, China na Iran zimesisitiza kuwa kuondoa vikwazo na kuhakikisha faida za kiuchumi za Iran ni sehemu muhimu ya mkataba huo na kwamba hilo litasaidia katika utekelezaji kamili wa makubaliano hayo.
Siku ya Jumanne, Beijing ilimpokea kwa heshima zote za kiitifaki Ebrahim Raisi ambaye alikuwa ameongonzana na wajumbe kadhaa wa kibiashara, katika ziara yake ya kwanza ya aina hiyo katika kipindi cha zaidi ya miaka 20.
Soma pia: China yaiahidi Iran uungwaji mkono thabiti
Shirika la utangazaji la serikali ya China CCTV limeripoti kuwa Xi alipongeza "mshikamano na ushirikiano" wa China na Iran katika kukabiliana na mabadiliko ya sasa ya ulimwengu, nyakati na historia.
Daima kwa mujibu wa shirika hilo, Xi amesema kuwa Beijing inaiunga mkono Iran katika masuala ya uhuru na kuyalinda mamlaka yake ya kitaifa, na kwamba inapinga msimamo wa uasi na uingiliaji wa majeshi ya kigeni katika masuala ya ndani ya Iran na kudhoofisha usalama na utulivu wa taifa hilo.
CCTV imebaini pia kuwa China na Iran zimetia saini nyaraka kadhaa za ushirikiano katika nyanja za kilimo, biashara, utalii, ulinzi wa mazingira, afya, misaada ya majanga, utamaduni na michezo.