1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Eritrea afanya ziara ya siku mili nchini Sudan

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
5 Mei 2021

Mara tu Rais huyo wa Eritrea Isaias Afwerki alipolakiwa kwenye uwanja wa ndege na Jenerali Abdel-Fattah Burhan, kiongozi wa baraza kuu linalotawala nchini Sudan moja kwa moja viongozi hao walianza mazungumzo ya faragha.

https://p.dw.com/p/3t0GK
Sudan Isaias Afwerki und Abdel Fatah al Burhan
Picha: Eritrea Minister of Information/Yemane G. Meskel

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Baraza Kuu linalotawala Sudan, mazungumzo ya viongozi hao wawili yanahusu ushirikiano na kutafuta njia za kukuza uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Taarifa hiyo pia ilitaja kwamba viongozi hao wawili walijadili juu ya masuala ya kikanda na hasa mvutano wa mpaka kati ya Ethiopia na Sudan pamoja na mzozo wa miaka kumi juu ya bwawa kubwa la umeme linalojengwa na Ethiopia kwenye Mto Nile.

Ziara hiyo ya siku mbili ya kiongozi wa Eritrea imefanyika baada ya Sudan mnamo mwezi Februari kutuhumu juu ya nchi ya tatu iliyosema inaiunga mkono Ethiopia katika mzozo wake wa mpaka na Sudan. Na tuhuma hizo bila shaka zilikuwa zinailenga Eritrea, ambayo imewapeleka wanajeshi wake kwenye eneo la Tigray kupigana pamoja na vikosi vya serikali ya Ethiopia katika mgogoro kwenye eneo hilo.

Soma Zaidi:Wanajeshi wa Eritrea waliingia Tigray-akiri Abiy Ahmed

Kufuatia tamko hilo la Sudan, Eritrea ilimtuma waziri wake wa mambo ya nje nchini Sudan ambaye alikwenda kuuhakikishia utawala wa mjini Khartoum kwamba Eritrea haikuwa sehemu ya mzozo kati ya Sudan na Ethiopia.

Mvutano kati ya Sudan na Ethiopia unahusu eneo kubwa la ardhi ya kilimo ambalo Sudan inasema ipo ndani ya mipaka yake katika eneo al-Fashqa ambalo wakulima wa Ethiopia wamekuwa wakilima kwa miaka mingi. Wakati huo huo, Sudan imesema mgogoro wa Tigray wa nchini Ethiopia, uliosababisha utitiri wa wakimbizi waliokimbia na kuingia nchini humo, umezidisha makali ya mzozo huo.

Rais wa Eritrea Isaias Afwerki na Rais wa Baraza Kuu linalotawala Sudan Abdel Fatah al Burhan
Rais wa Eritrea Isaias Afwerki na Rais wa Baraza Kuu linalotawala Sudan Abdel Fatah al BurhanPicha: Eritrea Minister of Information/Yemane G. Meskel

Ethiopia, nayo kwa upande wake inailaumu Sudan kwa kusema kuwa inautumia kama fursa mgogoro waTigray ambapo majeshi yake yanaingia katika eneo hilo la Ethiopia na kupora mali, kuua raia na kusababisha maelfu ya watu walikimbie eneo hilo la kaskazini magharibi mwa Ethiopia. Mapigano katika jimbo la Tigray yamesababisha wakimbizi zaidi ya 70,000 wa Ethiopia kukimbilia Sudan.

Wakati huo huo, madaktari wasiokuwa na mipaka wameelezea juu ya hali mbaya ya utapiamlo katika baadhi ya sehemu za mkoa wa Tigray uliokumbwa na vita nchini Ethiopia na wametahadharisha kwamba hali hiyo inaweza kuwa mbaya zaidi katika msimu unaokuja wa mvua.

Soma Zaidi:Mazungumzo kuhusu ujenzi wa bwawa la umeme la GERD yamekwama

Madaktari wa shirika hilo la msaada wa matibabu MSF, wamesema wakaazi wa maeneo hayo wanapata tabu kufika kwenye sehemu za kusambaza chakula na pia wamelalamika kwamba misaada hiyo haifiki katika maeneo ya vijijini katika jimbo la Tigray.

Mkuu wa idara ya msaada wa dharura ya shirika la MSF Karline Kleijer amesema kwenye taarifa yake kwamba kuna kiwango cha kutisha cha utapiamlo miongoni mwa watoto na akina mama wajawazito na wale  wanaonyonyesha wanaochunguzwa na wahudumu wa afya wa MSF wanaotembelea katika maeneo kadhaa katika mkoa wa kaskazini magharibi wa Tigray.

Vyanzo:AFP/AP