Mazungumzo kuhusu ujenzi wa bwawa la umeme la GERD yamekwama
6 Aprili 2021Hadi usiku kucha,mawaziri hao wameshindwa kufikia makubaliano. Duru kutoka ikulu ya rais Tshisekedi zinasema kwamba mazungumzo yamekwama kufuatia hasa vipingamizi vya Sudan. Lakini hata hivyo hazikufafanua kuhusu hatua iliyokwamisha mazungumzo hayo.
Juhudi za diplomasia za Umoja wa Afrika
Kwenye hafla ya ufunguzi wa mkutano huo, rais Felix Tshisekedi alizitolea mwito nchi hizo kuyapa kipau mbele maslahi ya wananchi wao. Na kuwahimiza wajumbe wote kwenye mkutano huo kufikia makubaliano ya kimsingi.
'' Tofauti kuhusu ujenzi wa bwawa la umeme la Ethiopia la Renaissance, haziwezi kuchukuliwa kama janga, bali kama fursa kwa ajili ya kuwaweka pamoja raia wetu na mwanzo mpya wa uhusiano wa mipakani na wa kikanda.'',alisema Tshisekedi.
Kulingana na ajenda ya mkutano huo wa Kinshasa,ni kwamba mawaziri hao wa mambo ya nje na wa umwagiliaji kutoka Misri,Sudan na Ethiopia watajadili masuala ya kiufundi na kisheria kuhusu ujenzi wa bwawa hilo la umeme kwenye mto Nile.
Kabla ya mkutano huo ,Sameh Shoukry, waziri wa mambo ya nje wa Misri,aliviambia vyombo vya habari vya nchi yake kwamba mkutano huo wa Kinshasa ni wamatumaini ya mwisho katika kufikia makubaliano .
Vitisho vya Misri na Sudan
Mazungumzo ya awali baina ya nchi hizo tatu ,chini ya upatanishi wa Umoja wa Afrika na rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, yalishindwa kutoa suluhu ya kudumu juu ya hatua ya Ethiopia ya kujenga bwawa kubwa la kuzalisha nishati ya umeme.
Ethiopia ilianza ujenzi wa bwawa hilo kwenye Blue Nile, mwaka 2010, kama sehemu ya mpango wa kupanua uuzaji wake wa nishati nje ya nchi.
Wiki iliopita Rais wa Misri, Abdel Fattah el-Sissi alionya juu ya hali ya kutokuwa na utulivu katika eneo hilo iwapo mradi huo wa Ethiopia utaendeshwa bila ya makubaliano ya kisheria.
el-Sissi amesema hakuna anayeweza kuchukua hata tone moja la maji kutoka Misri, na kumuonya yoyote anayetaka kufanya hivyo.
Rais huyo wa Misri hata hivyo, alisema nchi yake inaunga mkono mazungumzo juu ya kutatua mzozo uliopo kabla ya Ethiopia kuendelea na mchakato wa kujaza hifadhi kubwa ya bwawa wakati wa msimu wa mvua mwaka huu. Ethiopia ilianza kujaza bwawa hilo Julai mwaka uliopita, hatua ambayo ilikosolewa vikali na Misri na Sudan.