Rais wa Brazil hatimaye ajitokeza
22 Juni 2013Ameahidi kuimarisha huduma za umma na kufanya mazungumzo na viongozi wa maandamano.
Lakini bado haifahamiki hasa nani anaweza kuwakilisha makundi makubwa ambayo hayana uongozi ya waandamanaji wanaoingia mitaani, wakitoa hasira zao dhidi ya huduma mbovu za umma licha ya mzigo mkubwa wa kodi unaowakabili.
"Nitakutana na viongozi wa maandamano ya amani, nataka taasisi ambazo ziko wazi zaidi , zinaopinga matendo mabaya," Rousseff amesema akimaanisha hisia za rushwa katika siasa za Brazil, hali ambayo inajitokeza kama lengo la maandamano hayo. "Raia wake na sio uwezo wa kiuchumi ndio unapaswa kuwa mbele."
Waandamanaji wanataka huduma bora
Licha ya kuwa hakutoa maelezo zaidi , Rousseff amesema kuwa serikali yake itatengeneza mpango maalum wa kitaifa kwa ajili ya usafiri wa umma katika miji, kupanda kwa nauli za mabasi na treni za mijini lilikuwa ni lalamiko la msingi la waandamanaji.
Pia amerudia uungaji wake mkono wa mpango ulioko katika bunge la nchi hiyo kuwekeza mapato yote ya mafuta katika elimu na ahadi aliyoitoa hapo kabla ya kuwaleta madaktari kutoka nje katika maeneo ambayo yanakosa waganga.
Kiongozi huyo ambaye ni muasi wa zamani wa kundi la kikomunist ambaye amepambana dhidi ya utawala wa kijeshi wa Brazil mwaka 1964 hadi 1985 na alifungwa kwa muda wa miaka mitatu na kuteswa na utawala huo wa kijeshi, ameelezea kuhusu alivyojitolea muhanga hapo kabla kulifanya taifa hilo kuwa huru kutokana na utawala wa kidikteta.
"Kizazi changu kilipambana mno ili sauti katika mitaa ziweze kusikika," Rousseff amesema . "Wengi walishtakiwa, waliteswa na wengi wameuwawa kwa ajili hiyo. Sauti za mitaani ni lazima zisikike na kuheshimiwa na zinaweza kufikiriwa vibaya kwamba ni kelele na ghasia za baadhi ya watu wanaopenda kufanya ghasia.
Akosolewa
Amekosolewa kwa kiasi kikubwa kwa kutoonekana na kujali huku maandamano yakifanyika na kushindwa kuhusika na jamii ambayo inadai serikali yake iwasikilize.
Edvaldo Chaves , mwenye umri wa miaka 61 mlinzi wa nyumbani katika kitongoji kinachokaliwa na watu wenye uwezo kiasi cha Flamengo mjini Rio, amesema ameiona hotuba aliyotoa Rousseff siku ya Ijumaa kuwa inaridhisha.
"Nafikiri alikuwa mtulivu na alifanya kazi nzuri. Pamoja na kwamba , kwasababu alikuwa mpiganaji na aliishi uhamishoni , anazungumzia masuala ya waandamanaji kwa uhakika zaidi," Chaves amesema. "Nafikiri mambo yatatulia sasa. Huenda tutaendelea kuwaona watu mitaani lakini huenda itakuwa ni idadi ndogo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Bruce Amani