Watu milioni moja waandamana Brazil
21 Juni 2013Wimbi hilo la maandamano limeipiga karibu miji 80, na hapo jana karibu vurugu hizo ziuvuruge mchuano wa kombe la mabara mjini Rio De Janeiro. Hali hiyo imemfanya rais wa Bazil, Dilma Rouseff, kufuta ziara yake nchini Japan.
Maandamano makubwa zaidi yalifanyika mjini Rio De Janeiro, wakati takribani watu laki tatu walipokusanyika mjini humo jana, siku moja baada ya meya wa mji kutimiza masharti muhimu kwa kubatilisha uamuzi wa kuongeza nauli za usafiri wa umma. Maandamano hayo ya Rio yalianza kwa amani, huku waandamanaji wakitembea katikati ya mji huo kuelekea katika ofisi ya meya Eduardo Paes. Lakini ghasia zilizuka, huku polisi wakiwafyatulia mabomu ya kutoa machozi waandamanaji waliokuwa wakirusha mawe, na kuwajeruhi watu 30.
Gharama kubwa kwa ajili ya michezo
Waandamanaji wanalalamika kuhusu matumizi ya zaidi ya euro biioni 7.5 kazika maandalizi ya dimba la dunia mwaka 2014 wakisema pesa hizo ingekuwa vyema zitumiwe pengine. Maandamano hayo yalisambaa hadi mji mkuu Brasilia ambapo takribani watu 20,000 walitembea hadi mbele ya bunge. Waandamanaji walijaribu kuingia kwa nguvu katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Kigeni, na kulazimu makabiliano kati yao na polisi. Kulikuwa pia na umati wa watu katika mji wa Sao Paolo ambako maandamano hayo yalianzia, baada ya mji huo kuongeza nauli za mabasi na treni.
Karibu watu 110,000 walikusanyika katika mji mkubwa zaidi na kituo cha biashara nchini Brazil, Sao Paolo, ambako wimbi la sasa la maandamano lilianzia. Mwandamanaji mmoja aliuawa mjini humi, wakati gari lilipouginga umati wa waandamanaji. Mji huo ulikuwa umepandisha nauli za huduma za usafiri wa mabasi na matreni, na kuzusha maandamano ambayo yalienea kwa kasi kote nchini kupitia mitandao ya kijamii.
Rais Rousseff afuta safari
Rais wa Brazili, Dilma Rouseff, alilazimika jana kufuta ziara yake nchini Japan iliyopangwa kuanza Juni 26 hadi 28, ili kuyashughulikia maandamano hayo, ambayo ndiyo makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo tangu miaka 20 iliyopita.
Rousseff, mwanachama wa Chama cha Wafanyakazi kinachoegemea mrengo wa shoto, ameyakubali maandamano hayo. Mapema wiki hii, alisema kuwa waandamanaji “walikuwa wametuma ujumbe wa wazi kwa jamii nzima, na zaidi ya yote kwa viongozi wa kisiasa wa ngazi zote za serikali”. Lakini kufikia sasa, maneno yake ya kuunga mkono hayajafanya mechi kuwaridhisha wale wanaoandamana. Maandamano hayo yanafanyika wakati kinyang'anyiro cha kombe la mabara – Confederations Cup kikiendelea nchini humo. Brazil inajiandaa kwa dimba la Kombe la Dunia mwaka ujao pamoja na Michezo ya Olimpiki mwaka wa 2016.
Mwandishi: Bruce Amani/DW/DPA
Mhariri: Josephat Charo