Rais Mwinyi akutana na kikosi kazi cha demokrasia
20 Aprili 2022Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu Mjini Zanzibar, Rais Mwinyi alisisitiza maelekezo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ya kutaka mapendekezo yote yalyiotolewa na kikosi kazi hicho yafanyiwe kazi huku akiangazia maeneo makuu matatu muhimu, ikiwani ni pamoja na katiba mpya suala la utaratibu wa uchaguzi na hata mikutano ya hadhara na mikutano ya ndani.
Sambamba na hilo, Rais Mwinyi pia alitaka vyama vyengine vya siasa ambavyo vipo nje ya kikosi kazi hicho kuungana na wenzao ili kuharakisha juhudi za maelewano zinazoendelea kwa sababu kuwa na sauti moja kutasaidia kufikia malengo.
Chama cha upinzani chenye wafuasi wengi upande wa Tanzania Bara, CHADEMA, ni miongoni mwa vyama ambavyo havijajiunga na kikosi hicho kutokana na sababu mbalimbali, ukiwemo msimamo wao juu ya madai ya katiba mpya kucheleweshwa.
Kikosi kazi hicho kinachoongozwa na Profesa Rwekiza Mukandala kinachowajumuisha wanasiasa na wawakilishi wa makundi ya kiraia, wanahabari na asasi zisizo za kiserikali chini ya mwamvuli wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kiliundwa mwaka jana muda mfupi baada Rais Samia kuanza majukumu yake ya kazi ya urais, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake ya kufanya kazi kwa pamoja na vyama vya upinzani ili kuweka mazingira ya usawa katika siasa na kuheshimu demokrasia.
Wadadisi wa mambo wanasema huu ni mwelekeo mpya wa siasa nchini Tanzania baada ya miaka takribani sita chini ya utawala wa Marehemu John Magufuli, ambapo takribani shughuli zote muhimu za vyama vya siasa, uhuru na demokrasia viliwekwa kifungoni.
TCD, wakati huo ikiongozwa na Zitto Kabwe, kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, ambacho ni mshirika mdogo kwenye serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, ndiyo iliyofufua harakati za kuupa uhai wito wa Rais Samia kufanya kazi pamoja. Kwa sasa, nafasi ya uwenyekiti wa TCD inashikiliwa na Abdurahman Kinana, makamu mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara.
Mwandishi: Salma Said/DW Zanzibar