1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais aliyepinduliwa Sudan apelekwa jela mjini Khartoum

17 Aprili 2019

Rais aliyeondolewa kwa nguvu madarakani nchini Sudan Omar al-Bashir amehamishiwa katika jela ya Kobar iliyopo kwenye mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum. Taarifa hiyo imetolewa na duru mbili za familia.

https://p.dw.com/p/3GxXB
Sudan Omar Al-Bashir
Picha: Reuters/M. N. Abdallah

Duru nchini Sudan zimeliambia shirika la habari la Reuters kwamba Bashir alikuwa akishikiliwa chini ya ulinzi mkali katika makaazi ya rais baada ya kuondolewa kwake madarakani na jeshi Aprili 11.

Wakati huohuo waandamanaji bado wanaendelea kupiga kambi nje ya makao makuu ya jeshi wakitowa mwito wa kuundwa serikali ya kiraia na jeshi kujayakabidhi madaraka kwa amani.

Huku hayo yakiarifiwa waziri wa mambo ya nje wa Uganda amesema nchi hiyo iko tayari  kufikiria kumpa hifadhi rais aliyeondolewa madarakani nchini Sudan Omar al Bashir licha ya kiongozi huyo kutakiwa na mahakama ya kimataifa ya jinai ICC iliyoko mjini The Hague,Uholanzi.

Okello Oryem ameliambia shirika la Reuters kwamba Uganda haitoomba radhi kwa namna yoyote kwa kufikiria kuyakubalia maombi ya hifadhi ya bwana Bashir.