Qatar yasema ina matumaini katika mazungumzo mapya ya Doha
19 Machi 2024Kwanza kabisa Majed al-Ansari aliwaambia waandishi habari mjini Doha kwamba wapo katika wakati ambapo hawawezi kusema wanakaribia kufikia makubaliano ya kusitishwa mapigano. Amesema kitu wanachojua ni kwamba kuna matumaini hayo baada ya majadiliano hayo kuanza tena, na hilo ni jambo zuri wanalotumai litaendelea. Amesema kwa sasa ni mapema mno kutangaza mafanikio ya aina yoyote lakini wanabakia kuwa na matumaini.
Alipoulizwa iwapo ajenda ya usitishwaji kabisa mapigano ipo katika meza ya mazungumzo, alisema kilicho muhimu kwa sasa ni usitishwaji mapigano kwa muda ili misaada ya kiutu iweze kufikishwa kwa watu wa Gaza wanaokabiliwa na njaa.
"Tumezungumza kwa uwazi kabisa kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa. Kwanza ni kusitisha mapigano kwaajili ya kupitisha misaada ya kiutu, tukifanikiwa kwa hilo, tutasimamisha mateso, tutahakikisha kuna hatua za kubadilisha wafungwa na matekwa walioshikiliwa na mambo mengi ambayo mmeshayajadili. Na baadae tunatumai tutakwenda katika hatua ya pili ya kusitisha kabisa mapigano. Ila kwa sasa tunataka mapigano yasitishwe kwaajili ya misaada ya kibinaadamu kufikishwa Gaza kwanza," alisema Majed al-Ansari.
Antony Blinken asema hali ya Gaza inazidi kuwa mbaya
David Barnea Mkuu wa shirika la ujasusi la Israel Mossad, aliondoka nchini Qatar baada ya mazungumzo lakini ujumbe wa Israel wakiwemo wawakilishi wa ujasusi wa ndani na jeshi la ulinzi bado upo Qatar kushiriki mazungumzo hayo. Matarajio ni kwamba mazungumzo yanayohudhuriwa na wawakilishi wa Misri, Marekani na Wenyeji Qatar yataendelea kwa wiki moja au mbili zijazo.
Mashambulizi yanayofanyika Rafah huenda yakayatia doa mazungumzo ya Qatar
Hata hivyo Qatar ambayo ni mpatanishi katika mazungumzo ya kusitishwa vita kati ya Israel na Hamas, kupitia msemaji wake Majed al-Ansari, imeonya pia kwamba mashambulizi yanayofanywa na jeshi la Israel mjini Rafah kusini mwa Gaza huenda yakayumbisha hatua za kufikiwa makubaliano.
"Tumetahadharisha na bado tunatahadharisha, kuwa shambulizi lolote mjini Rafah kutafanya hali ya kibinaadamu kuwa mbaya zaidi na pia kutasababisha mateso ambayo hayajawahi kuonekana katika mgogoro huu," alisema Al Ansari.
Lakini Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema operesheni ya ardhini inahitajika mjini Rafah ili kulitokomeza kundi la wanamgambo wa Hamas mjini humo. Kauli yake ameitoa kufuatia wito uliotolewa na Marekani wa Israel kufikiria upya mkakati wake huo mpakani mwa Gaza walikojazana wapalestina waliopoteza makaazi yao. Aliwaambia wabunge wake kwamba alimueleza kwa uwazi rais wa Marekani Joe Biden kwamba wamejitolea kuwatokomeza Hamas mjini Rafa na hakuna njia nyengine isipokuwa operesheni ya ardhini.
Israel inawasaka tena Hamas katika hospitali ya Shifa
Huku hayo yakiarifiwa Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk, amesema Israel ikiendelea kudhibiti msaada wa kibinaadamu unaoingia Gaza huenda ikatafsiriwa kama kutumia njaa kama silaha hatua inayoweza kuchukuliwa kama uhalifu wa kivita. Kwengineko bunge la Canada limepitisha muswada usiokuwa na nguvu ya kisheria unaotoa wito kwa Jumuiya ya kimataifa kufanyakazi kuelelea suluhu ya mataifa mawili ili kuutatua mgogoro kati ya Israel na Palestina.
ap/reuters/afp