1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin:Wasyria ndio wanaoweza kuamua mustakabali wa nchi yao

30 Januari 2018

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema raia wa Syria wanapaswa kushikamana na kuwa na maono ya pamoja juu ya mustakabali wao wa baadaye ili kukabiliana na mgogoro unaoendelea nchini mwao.

https://p.dw.com/p/2rmPn
Russland Syrien Gespräche in Sotschi Rede Außenminister Lawrow
Picha: Reuters/S. Karpukhin

Akisoma ujumbe kutoka kwa rais Putin Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema mikakati fulani imewekwa kuufungua ukurasa mpya katika historia ya Syria, akisema ni wasyria wenyewe ndio wanaoweza kuamua mustakabali wa nchi yao. Katika mkutano huo kulikuwa na wawakilishi wa makabila tofauti makundi ya kijamii na kisiasa. Aidha Lavrov ameishukuru Uturuki, Iran na Umoja wa Mataifa kwa kuunga mkono mazungumzo ya amani ya Syria.

Hata hivyo baadhi ya wajumbe katika mkutano huo walisimama na kumzomea Sergei Lavrov wakati alipokuwa anatoa hotuba yake, wakiishutumu Urusi kwa mauaji ya raia nchini Syria kwa mashambulizi yake ya angani. Tukio hilo pia lilionyeshwa moja kwa moja kupitia televisheni ya kitaifa ya Urusi ambapo maafisa wawili walionyeshwa wakimfuata mtu mmoja katika mkutano huo na kumtaka akae chini na kunyamaza.

Wajumbe wengine katika mkutano huo mjini Sochi waliamka wakati mmoja na kupaza sauti ya kuiunga mkono Urusi. Lavrov aliwataka wajumbe kukaa chini na kummpa nafasi ya kumaliza hotuba yake huku akiwaambia watakuwa na muda wao wa kuzungumza baadaye katika mkutano huo.

Baadhi ya wajumbe wa upinzani wasusia mkutano wa amani wakidai matakwa yao hayajatekelezwa

Syrien-Konferenz in Sotschi
Baadhi ya wajumbe katika mkutano wa kutafuta amani ya Syria mjini SochiPicha: Reuters/S. Karpukhin

Huku hayo yakiarifiwa kiongozi wa wajumbe wa upinzani Ahmed Tomah amesema wameamua kuususia mkutano wa amani wa Syria baada ya ahadi zilizotolewa kutotekelezwa kama kusitisha mashambulizi ya angani yanayofanywa na Urusi na kuondoa nembo za serikali ya Syria.

Ndani ya Syria kwenyewe mashambulizi mengine ya angani yanayofanywa na Uturuki yamelitikisa eneo la mpakani mwa Syria la Afrin huku mapigano yakizidi katika maeneo mengine, wakati Uturuki ikiendelea kupambana dhidi ya kundi la wapiganaji wa kikurdi.  Kundi la uangalizi pamoja na duru kutoka kwa wakurdi zinasema operesheni za kijeshi za Uturuki zimeshika kasi katika siku yake ya 10 ya mashambulizi dhidi ya wapiganaji hao Kaskazini Magharibi mwa Syria.

Hapo jana mamia ya watu walihudhuria mazishi ya pamoja ya raia na wapiganaji waliyouwawa mjini Afrin, watu hao walionekana kububujikwa na machozi huku wakibeba majeneza yaliyofunikwa kwa bendera ya wapiganaji wa kikurdi. Waangalizi wanasema watu 67 wameuwawa tangu operesheni dhidi ya wapiganaji wa wakurdi kuanza mnamo januari 20. Kwa upande wake Uturuki inakanusha vikali madai ya kusababisha vifo vya raia ikisema inajaribu kila iwezalo kuepuka mauaji ya raia katika operesheni zake.

Takriban watu 340,000 wameuwawa tangu vita vya wenyewe kwa wenyea kuanaza nchini humo mwaka 2011.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/Reuters/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman