1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin: Nchi za Magharibi haziwezi kuizuia China kuendelea

12 Septemba 2023

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema leo kuwa juhudi za nchi za Magharibi za "kuizuia" China kuwa taifa lenye nguvu kubwa kimataifa hazitofanikiwa, na amesifu uhusiano mzuri kati ya Urusi na China.

https://p.dw.com/p/4WFwv
Rais wa Urusi Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Vyacheslav Viktorov/AP/picture alliance

Akizungumza kwenye kongamano la uchumi katika mji wa mashariki mwa Urusi wa Vladivostok ambapo China imetuma wajumbe wake, Putin amesema ushirikiano kati ya Moscow na Beijing katika sekta za ulinzi na usalama unaendelea kushamiri.

"Leo nchi za Magharibi zinajaribu kuzuia maendeleo ya China kwa sababu chini ya uongozi wa rafiki yetu Xi Jinping, China inapiga hatua kubwa za maendeleo." Alisema Putin.

Aliongeza kwenye hotuba yake kwamba hali hiyo inawashtua wengi na kuna jitihada za kila namna katika kupunguza kasi ya maendeleo ya China.

Soma pia:Putin: Operesheni ya Ukraine haijapata mafanikio

Urusi imejikita zaidi katika kuimarisha uhusiano wa kibiashara, nishati na kijeshi na China baada ya uamuzi wake wa kuivamia Ukraine mnamo Februari 24 mwaka jana, hatua iliyosababisha kudorora kwa uhusiano wake na nchi za Magharibi. 

China imekataa kuilaumu Urusi kwa vita vya Ukraine na badala yake imekosoa vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi kwa Urusi.