Kim Jong Un awasili Urusi kwa mkutano na rais Putin
12 Septemba 2023Kim amewasili nchini Urusi kwa ziara ya nadra nje ya nchi siku moja baada ya mataifa hayo mawili kuthibitisha uvumi kuwa kiongozi huyo wa Korea Kaskazini atakutana na Vladimir Putin katika siku za karibuni.
Mkutano huo litakuwa jukwaa kwa kila upande kuonesha uungaaji mkono kwa mwingine.
Treni ya kisasa ya rangi ya kijani kikavu iliyonakshiwa kwa ufito wa rangi ya dhahabu ilivuka mvuka wa Korea Kaskazini na kuingia upande wa mashariki wa Urusi ikiwa imembeba Kim na ujumbe wake.
Iliondoka Pyongyang, mjini mkuu wa Korea Kaskazini siku ya Jumapili, ambapo Kim aliagwa kwa heshima kubwa na maafisa wake wa ngazi ya juu. Picha hizo za kuanza safari zimetolewa leo na shirika la habari la taifa hilo.
Eneo la mkutano wa Kim na Putin bado halijulikani
Kiongozi huyo anatarajiwa kukutana na Putin katika eneo ambalo hadi sasa halitajwa lakini inaaminika itakuwa ni upande wa mashariki ya mbali nchini Urusi.
Rais Vladimir Putin hivi sasa yuko kwenye mji wa Vladivostok ulio jirani na Korea Kaskazini kuhudhuria Jukwaa la Kiuchumi la Mataifa ya Mashariki.
Hata hivyo hakuna ishara kwamba Putin atakutana na Kim kwenye eneo hilo. Duru zinasema Putin anapanga kusafiri kwenda eneo jingine liitwalo Vostochny Cosmodrome na huku ndiyo pengine atakutana na Kim.
Kwenye hotuba yake na hata mjadala wa wazi kwenye mkutano wa Vladivostok, Putin hajasema neno hata moja kuhusu mkutano wake na Kim.
Badala yake amerejea matamshi yake ya kuyalaumu mataifa ya magharibi kwa hali dhaifu ya uchumi duniani na matatizo mengine yanayoukabili ulimwengu.
"Sote tunafahamu, sote tunaona jinsi uchumi wa dunia ulivyobadilika na unavyoendelea kubadilika miaka ya karibuni, na pia hilo ni kutokana na ukweli kwamba baadhi ya mataifa, hususani ya magharibi, ndiyo yanaharibu kwa mikono yao wenyewe mfumo wa kifedha, biashara na ushirikiano wa kiuchumi ambao waliubuni na kuupigia chapuo"
Kuipatia Urusi silaha inatarajiwa kuwa ajenda ya juu mkutano wa Kim na Putin
Ama juu ya mkutano wake na Kim, wafuatiliaji wanasema Putin huenda ataomba kupatiwa mabomu na makombora ya kuchakaza vifaru vya kivita kutoka Korea Kaskazini huku Pyongyang itaweka mezani maombi ya kupatiwa msaada wa teknolojia ili kuunda satelaiti ya kisasa na nyambizi zinatotumia nishati ya nyuklia.
Marekani ambayo wiki iliyopita ndiyo ilidokeza kwa mara ya kwanza mipango ya mkutano wa Kim na Putin imeitahadharisha Korea Kaskazini kuwa "italipa" iwapo itaipatia Urusi silaha kwa ajili ya vita nchini Ukraine.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani Matthew Miller, amesema Washington itafuatilia kwa karibu mkutano wa viongozi hao wawili na imezikumbusha nchi zote mbili kwamba "upelekaji wowote wa silaha za Korea Kaskazini nchini Urusi, utakuwa ni ukiukaji wa maazimio kadhaa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa"
Baada ya miongo kadhaa ya mahusiano ya panda shuka, Urusi na Korea Kaskazini zimejongeleana sana tangu Moscow ilipotuma vikosi vyake nchini Ukraine mwaka 2022.
Mshakamano wao unaotokana na dhamira ya Kim ya kuimarisha mahusiano na washirika wake wa jadi ambao ni Urusi na China wakati anajaribu kujitoa kimasomaso mbele ya shinikizo kubwa la kutengwa kimataifa.