Putin atia saini sheria inayomuezesha kuongoza hadi 2036
6 Aprili 2021Mabadiliko hayo ya katiba yaliofanyika Julai mosi mwaka jana, yanajumuisha kipengele kilichobadilisha mihula ya rais na kumruhusu Putin, kuendelea kuwania urais kwa mihula mingine miwili.
Sheria hiyo mpya iliyotangazwa hapo jana iliidhinishwa na bunge la Kremlin linalodhibitiwa na serikali, kabla ya kuwekwa wazi katika ukurasa rasmi wa serikali wa masuala ya sheria za taifa.
soma zaidi: Urusi yafanya kura ya maoni ya kubadilisha katiba
Rais Putin aliye na miaka 68 ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miongo miwili, na kuwa rais aliyekaa muda mrefu uongozini tangu kuondoka kwa dikteta Josep Stalin, amesema ataamua hapo baade iwapo atagombea tena mwaka 2024 wakati muhula wake wa miaka sita utakapomalizika.
Amesema kubadilisha mihula ya uongozi ni kitu kilichohitajika ili kuendelea kuwaongoza wajumbe wake kuwa makini kazini kuliko kuanza kutafuta mtu atakaemrithi.
Hata hivyo wakosoaji wanasema mabadiliko ya katiba yalifanywa kwa maksudi ili kumfungulia Putin njia ya kuongoza milele. Putin atakuwa na miaka 83 au 84 iwapo ataendelea kuiongoza Urusi hadi mwaka 2036.
Sheria hiyo iliyotangazwa hapo jana pia imetoa matakwa mapya kwa mgombea wa Urais kwamba ni lazima awe zaidi ya miaka 35, awe mkaazi wa Urusi kwa miaka 25 na mtu ambaye hajawahi kuwa na uraia wa kigeni au kuwa na kibali cha kukaa milele katika nchi nyengine isipokuwa Urusi.
Sheria yatiwa saini wakati seriali ikidaiwa kuwakandamiza wapinzani
Sheria hiyo imekuja huku serikali ikikosolewa kwa namna inavyowakandamiza wapinzani na wakosoaji wake, ikiwemo kumfunga jela kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini humo Alexei Navalny.
Navalny ambaye ni mkosoaji wa serikali ya Vladimir Putin aliye na miaka 44 alikamatwa alipokuwa anarejea nchini kutoka Ujerumani alikokuwa anapokea matibabu kwa miezi mitano baada ya kupewa sumu, anayodai ilitoka kwa serikali ya Urusi. Serikali ya Urusi imeendelea kukanusha madai hayo.
soma zaidi:Amnesty Intl: Navalny sio mfungwa mwenye dhamira ya dhati
Mwezi Febriari alihukumiwa kifungo cha miaka miwili na nusu kwa makosa ya ubadhirifu, Navanly alikanusha madai hayo akisema yamepangwa dhidi yake.
Mawakili wake wamesema amekonda mno kutokana na hatua yake ya kuamua kususia chakula ili kushinikiza kupewa huduma bora ya matibabu akiwa gerezani.
Chanzo: afp,reuters