Purukushani zaigubika Ugiriki
20 Oktoba 2011Purukushani hizo zilitokea pindi baada ya bunge la Ugiriki kuiidhinisha miswada mipya itakayoiwezesha serikali kubana matumizi kwa kiasi kikubwa zaidi. Hata hivyo, miswada hiyo inasubiri kuidhinishwa rasmi katika kura ya pili itakayopigwa hii leo.
Mgomo na Mikato
Vurumai hizo za Jumatano jioni zilitokea wakati ambapo mgomo wa kitaifa utakaodumu kwa muda wa saa 48 ulipokuwa ukianza. Taarifa zinaeleza kuwa huduma muhimu zilikwamishwa kote nchini Ugiriki kwasababu ya mgomo huo.
Kulingana na miswada hiyo mipya, raia wa Ugiriki watalazimika kulipa kodi zaidi, kupunguziwa malipo yao ya uzeeni pamoja na mishahara, kadhalika kusimamishiwa kwa muda malipo ya mishahara iliyopunguzwa ya wafanyakazi alfu 30 vilevile kuisitisha mikataba mipya.
Punguzo kwa kila sekta
Serikali ya Ugiriki imelazimika kuichukua hatua hiyo kabla ya kupokea mikopo zaidi kati ya fungu la euro bilioni 110 ilizoahidiwa na serikali za mataifa ya Ulaya pamoja na Shirika la Fedha Ulimwenguni, IMF. Kwa upande wake, uongozi wa Ugiriki umesisitiza kuwa hautakuwa na fedha zozote endapo hautopokea kiasi ya euro bilioni 8 za mwanzo, jambo linalopingwa na Wagiriki. Waziri wa Fedha wa Ugiriki, Evangelos Venizelos anashikilia kuwa suluhu ni kukabiliana na hali hiyo ngumu.
Mwandishi: Mwadzaya, Thelma-ZPR
Mhariri: Mtulya, Abdul