Waandamanaji wapambana na polisi Ugiriki
19 Oktoba 2011Kwa mara ya kwanza kabisa tangu mzozo wa Ugiriki kuibuka miaka miwili iliyopita, waandamanaji leo wamejipenyeza hadi kwenye ngazi za jengo la bunge. Waziri Mkuu George Papandreou aliepoteza umaarufu wake, ametoa mwito kwa wananchi wake kuziunga mkono hatua mpya za kubana matumizi. Miongoni mwa hatua hizo, ni kupandisha malipo ya kodi, kushusha mishahara na kupunguza idadi ya wafanyakazi katika sekta ya umma. Waandamanaji wenye hasira na waliyochoshwa na mipango ya kubana matumizi mara kwa mara, wamekusanyika kwa maelfu kwenye Uwanja wa Syntagma katikati ya mji mkuu Athens kuanzisha mgomo mkuu wa siku mbili.
Polisi waliokuwa wakililinda jengo la bunge wametumia mabomu ya kutoa machozi baada ya polisi hao kushambuliwa na waandamanaji kwa mawe na mabomu ya petroli. Zaidi ya polisi 7,000 wametawanywa barabarani kuzuia machafuko. Hata hivyo maandamano hayo yametumiwa na makundi madogo ya wafanya ghasia kufanya uharibifu mbele ya hoteli za anasa na maduka makubwa. Katika mji mkubwa wa pili Thessaloniki, kiasi ya waandamanaji 100 wameshambulia makao makuu ya serikali ya mkoani na watu kadhaa wamejeruhiwa.
Mapamabano yaliyotokea, yametia doa mgomo uliyosababisha idara za serikali na maduka kufungwa na kusitisha huduma za kijamii. Kiasi ya safari za ndege 159 zimefutwa. Kwa mujibu wa polisi, zaidi ya watu 125,000 wanaandamana kote nchini humo, kuupinga mswada mpya wa kupunguza matumizi unaojadiliwa bungeni kabla ya sehemu ya mpango huo kupigiwa kura baadae leo hii. Kura ya pili kuhusu vipengele maalum, itapigwa kesho Alkhamisi.
Viongozi wa kimataifa, wanaotoa msaada wa fedha kwa Ugiriki, wanapoteza subira na kuzorota kwa mchakato wa mageuzi wa serikali ya nchi hiyo, ambayo haikutekeleza malengo ya kudhibiti bajeti yake. Sauti zinazidi kupazwa kuitaka serikali ya Ugiriki iwe chini ya usimamizi mkali wa Umoja wa Ulaya ili kuhakikisha kuwa itawajibika kutekeleza mageuzi yanayohitajiwa.
Mwandishi: Martin,Prema/rtre
Mhariri: Yusuf Saumu