Poland yachukuwa uraisi wa Umoja wa Ulaya
30 Juni 2011Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, Radoslaw Sikorski, amewaambia waandishi wa habari kwamba jukumu muhimu la nchi yake katika Umoja wa Ulaya litakuwa ni kuimarisha mshikamano wa mataifa ya Ulaya, ambao hivi sasa umetikiswa kutokana na mgogoro wa madeni wa Ugiriki.
Poland yenyewe si mwanachama wa nchi zinazotumia sarafu ya Éuro lakini, kwa mujibu wa Sikorski, inajiona ina wajibu wa kutumia nafasi yake ya uongozi wa Umoja wa Ulaya, kuyasaidia mataifa wanachama ambayo yamepigika vikali kwa mgogoro wa kifedha, ikiwemo Ugiriki.
"Kipaumbele chetu cha kwanza ni kuanzisha tena ukuwaji wa uchumi barani Ulaya, kwani tunaamini kuwa ni kutokana na hilo tu, ndipo mengine yatakapoweza kufuatia, kwa maana ya mshikamano zaidi, ukaribu mkubwa zaidi kwa majirani, na uwazi zaidi kwa utanuzi wa jumuiya." Amesema Sikorski.
Waziri huyo wa Mambo ya Nje ameahidi kuwa nchi yake itatumia uzoefu wake katika masuala ya madeni, ambao unatajwa kuisadia nchi hiyo kuepuka kuserereka kiuchumi kama yalivyo mataifa mengine ya Ulaya yanayofanana nayo.
Poland imeweka sheria ya kudhibiti madeni ya serikali, ambapo kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, deni halipaswi kuwa zaidi ya asilimia 60 ya uzalishaji wa pato la taifa.
Hata hivyo, Alhamis (30.06.2011) maelfu wa wanaharakati wa vyama vya wafanyakazi walifanya maandamano katika mji mkuu wa Warsaw, wakiishutumu serikali ya nchi hiyo kwa kuyatenga matatizo ya kijamii na kiuchumi.
Mkuu wa Mshikamano wa Wafanyakazi, Piotr Duda, aliwaambia waandishi wa habari kwamba Umoja wake unataka ongezeko la mishahara ya kima cha chini, punguzo la kodi ya mafuta na urahisi katika mafao ya ustawi wa jamii.
Waandamanaji hao walijikusanya kwenye uwanja wa Pilsudski, uliopo katikati ya Warsaw, kabla hawajaandamana kupitia bungeni na ofisi za serikali. Moja ya mabango ya waandamanaji hao lilisomeka: "Nyinyi munacheza siasa, sisi tunateseka", huku waandamanaji wakiimba kwa kusema: "Tunajua munatudanganya."
Mshikamano wa Wafanyakazi wa Poland unatambuliwa kimataifa kama injini nyuma ya mapinduzi ya umma dhidi ya utawala wa Kikomunsiti hapo mwaka 1989.
Hata hivyo, kwa sasa vuguvugu halisi la Mshikamano huo limegawika katika makundi mbali mbali ya kisiasa, huku tawi lake lililobakia likiendelea kutoa upinzani mkali kwa serikali ya Waziri Mkuu, Donald Tusk, ambaye hata yeye mwenyewe aliwahi kuwa mwanaharakati wa Mshikamano.
Miongoni mwa masuala makubwa yanayopiganiwa na Mshikamano wa Wafanyakazi ni kupanda kwa bei za vyakula na ongezeko la watu wasiokuwa na ajira, ambapo kiasi ya asilimia 12 ya raia wa Poland hawana kazi, ingawa ni nchi pekee katika Umoja wa Ulaya ambayo uchumi wake haukutikisika wakati wa mgogoro wa kifedha ulimwenguni.
Poland, ambayo yenyewe ilijiunga na Umoja wa Ulaya hapo mwaka 2004, imesema kwamba itapigania pia kutanuliwa kwa Umoja huo, ikiwemo kufanya mazungumzo ya uwanachama wa Croatia kabla ya mwishoni mwa mwaka huu.
Baada ya miaka sita ya mazungumzo mazito, Ijumaa iliyopita Umoja wa Ulaya uliamua mjini Brussels kwamba hatua za haraka zichukuliwe ili kukamilisha maafikiano ya uwanachama wa Croatia kufikia mwishoni mwa Juni 2011.
Mkutano wa mwezi Septemba 2011, ambao utafanyika mjini Warsaw, unatarajiwa kukamilisha hatua za mwisho za Ukraine nayo kujiunga na Umoja huo na makubaliano ya kibiashara.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman