Ugiriki kusaidiwa na Umoja wa Ulaya kwa masharti
24 Juni 2011Wakati wa mkutano huo wa kilele wa siku mbili mjini Brussels, serikali ya Ugiriki iliomba rasmi msaada wa fedha. Lakini bunge la Ugiriki linapaswa kuidhinisha mpango mpya wa kubana matumizi kabla ya mwisho wa mwezi huu, ili mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro katika Umoja wa Ulaya, wapate kukamilisha vipengele kadha. Baadae mawaziri hao wa fedha wataweza kupitisha maamuzi yanayohitajiwa hadi mwanzoni mwa mwezi Julai.
Rais wa Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy amesema, msaada huo mpya utasaidia kukidhi mahitaji ya Ugiriki katika mwezi wa Julai. Hicho ni kitita cha Euro bilioni 12 zinazohitajiwa na Ugiriki mwezi ujao, ili isipate kufilisika. Fungu hilo la fedha ni kutoka mkopo wa Euro bilioni 110 uliodhaminiwa mwaka uliopita na nchi za kanda ya Euro katika Umoja wa Ulaya pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF. Fungu hilo la fedha limezuiliwa mpaka bunge la Ugiriki litakapoidhinisha mpango mpya wa kubana matumizi. Kuambatana na mpango huo, serikali ya Ugiriki inapaswa kupunguza matumizi yake kwa Euro bilioni 28 zingine na kuuza mali ya taifa yenye thamani ya Euro bilioni 50. Mpango huo lakini unapingwa vikali na baadhi ya wananchi.
Hata hivyo, viongozi wa Umoja wa Ulaya wametoa mwito kwa vyama vyote vya kisiasa nchini Ugiriki kuunga mkono mpango huo. Wamesema, mafanikio ya mpango huo, yanategemea umoja wa kitaifa. Nae Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema, vyama vyote vya kisiasa nchini Ureno na Ireland vilishikamana ili kutekeleza mageuzi muhimu ya kupunguza matumizi ya serikali. Akaongezea:
" Na kuhusu Ugiriki, vyama vya upinzani nchini humo pia, vinatolewa mwito wa kutekeleza wajibu wake wa kihistoria."
Serikali ya kisoshalisti ya Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou ina wingi wa viti vitano tu bungeni. Hiyo jana vyama vya wafanyakazi nchini humo vilitangaza mgomo mkuu kuanzia Jumanne ijayo, siku ambayo bunge litapiga kura kuhusu mpango wa kubana matumizi. Mzozo wa madeni ya Ugiriki unaweza kuvuruga mfumo mzima wa sarafu ya Euro. Kwa hivyo, mwenyekiti wa kundi la nchi zinazotumia sarafu ya Euro, Jean-Claude Juncker anaetaka kuona mpango huo ukifanikiwa amesema:
"Hakuna mpango mwingine. Ugiriki haina budi kuchukua hatua zinazohitajika, halafu sisi pia, tutatimiza kile tunachopaswa kufanya."
Siku ya pili ya mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya leo, utashughulikia masuala ya Libya na Syria. Mada ya wakimbizi na udhibiti wa mipaka kati ya nchi zilizoondoa vituo vyake vya ukaguzi mpakani, kuambatana na makubaliano ya Schengen pamoja na uanachama wa Kroatia katika Umoja wa Ulaya ni masuala mengine katika ajenda ya mkutano wa Brussels.
Mwandishi:Hasselbach,Christopher/ZPR/P.Martin/afpe,afpd
Mhariri: Hamidou, Oumilkheir