Pakistan yazidi kuwaandama Wataliban
18 Desemba 2014Jitihada hiyo imechochewa na shambulio la kigaidi la jumanne lililosababisha vifo vya takribani watu 148 wengi wao wakiwa wanafunzi.
Ndege za kijeshi zimeshambulia maficho 20 ya wanamgambo hao ya katika wilaya ya kikabila ya Khyber iliyopo mji wa Peshawar, ambako wanamgambo wa Taliban Jumanne iliyopita walifanya mashambulizi yaliyosababisha vifo vya watu watu 148, wakiwemo wanafunzi 135 katika shule inayiomilikiwa na jeshi.
Majeshi ya ardhini yanafanya kazi bega kwa bega
Taarifa ya jeshi la nchi hiyo inaeleza kuwa majeshi ya ardhini pia yamesonga mbele na kuingia katika maeneo ya ndani zaidi katika eneo la bonde la Tirah, eneo lenye milima karibu na mpaka na Afghanistan ambako makundi kadhaa ya wanamgambo yenye mafungamano na kundi la al-Qaeda yamejihimarisha kwa kuweka makazi yao huko.
Katika operesheni tofauti askari wa Pakistan wamewauwa wanamgambo watano wanaoshukiwa kuwa ni Taliban katika mji wa kusini wa bandari ya wa Karachi. Taarifa hizo ni kwa mujibu wa msemaji wa kikosi hicho.
Hali ya utulivu yarejea Peshawar
Hali ya kawaida imeanza kurejea taratibu katika mji wa Mjini Peshawar baada kukaribia karibu kushindwa kuendelea na shughuli zake za kawaida hapo jana wakati wa maombolezo ya shambulio baya kabisa kuwahi kushuhudiwa nchini Pakistan kwa zaidi ya muongo mmoja.
Katika mji mkuu wa Islamabad, wanasiasa na viongozi wa jeshi wameanzisha mjadala wa wazi wenye shabaha ya kile walichokiita "mjadala wa mpango mpya wa kukabiliana na wanamgambo"
Waziri Mkuu Sharif aapa kuangamiza ugaidi
Katika mkutano huo, Waziri Mkuu Nawaz Sharif aliapa kuyasambaratisha makundi ya wanamgambo wa Kiislamu kwa kutumia nguvu zote za kijeshi na na kuamua mara moja kumalizika kwa miaka sita kusitisha kunyonga kwa waliokutwa na hatia ya ugaidi.
Maelfu ya raia wa Pakistan waliingia mitaani katika miji yote mikubwa kulaani shambulizi hilo lililouwa watu wengi na kuishinikiza serikali kuchukua hatua madhubuti dhidi ya wanamgambo nchini humo.
Mwandishi: Sudi Mnette DPAE/CCTV
Mhariri: Yusuf Saumu