Pakistan yaomboleza mauwaji ya watoto 142
17 Desemba 2014Sala za maiti zimefanyika kote nchini na katika shule huku wanafunzi wakielezea jinsi walivyopata mshituko kutokana na mauwaji hayo ambapo wanamgambo sabaa wa Taliban waliojifunga miripuko viunoni walivyoparamia ukuta na kuingia katika shule hiyo inayosimamiwa na jeshi .
Wanafunzi walipigwa risasi na baadhi ya waalimu wakike walitiwa moto wakiwa hai.
Serikali imetangaza siku tatu za msiba kuanzia leo.Mazishi yameanza tangu jana usiku lakini yale ya wanafunzi 132 na waalimu na watumishi wengine 10 wa shule hiyo yanafanyika leo.Wanafunzi wengine 121 na waalimu wengine watatu wamejeruhiwa.
Makatili hawana Dini
"Wametumia dakika tu kuangamiza kilicho muhimu nilichotumia maisha yangu yote kukiimarisha,mwanangu wa kiume" amesema Akhtar Hussain,anaefanya kazi ya kibarua huku machozi yakimtiririka,alipokuwa anamzika mwanawe mwenye umri wa miaka 14,Fahad .
Mwenzake Mohammed Saleem anasema:"Msiba mkubwa huu kwetu sote.Hakuna sio sisi waislam na hata wale ambao si waislam anaeuwa watoto.Hawana dini yoyote hawa."
Shambulio hilo limelaaniwa na ulimwengu mzima.Hata wanamgambo wa Taliban katika nchi jirani ya Afghanistan wamelaani mauwaji hayo na kusema hayaambatani na mwongozo wa dini ya kiislam.
Serikali ya waziri mkuu Nawaz Sharif imesema inapanga kurejesha tena adhabu ya kifo kwa kadhia zinazohusiana na ugaidi.Sheria hiyo ya adhabu ya kifo ilibatilishwa tangu mwaka 2008.Tangu wakati huo mtu mmoja tu ndie aliyeuliwa,mwanajeshi aliyekutikana na hatia na korti ya kijeshi na kunyongwa novemba mwaka 2012.
Waziri mkuu Nawaz Shariff ameahidi kuendelea na opereshini za kijeshi wakisaidiwa na ndege zisizokuwa na rubani za kimarekani dhidi ya wanamgambo wa Taliban.
"Tutazingatia kila tone la damu la watoto wetu"amesema waziri mkuu wa Pakistan kabla ya kukimbilia Peshawar hapo jana .
Wahanga wa Peshawar wanakumbukwa pia India
Katika nchi jirani ya India ambako viongozi daima walikuwa wakiituhumu Pakistan kuwaunga mkono wapiganaji wa chini kwa chini wanaoipinga serikali ya New Delhi,wanafunzi katika shule zote walikaa kimya dakika mbili hii leo kuomboleza mauwaji ya wanafunzi wenzao wa Peshawar.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/AFP
Mhariri: Gakuba Daniel