1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Oxfam: ukosefu wa usawa waongezeka

11 Oktoba 2022

Shirika la Oxfam limefichua matokeo ya utafiti wake wa "Ahadi ya kupunguza kiwango cha ukosefu wa usawa" (CRI), na kuchunguza hatua za serikali kukabiliana na ukosefu wa usawa wakati wa janga la virus vya corona.

https://p.dw.com/p/4I1tP
OXFAM Logo
Picha: AP Graphics

Ripoti hiyo iinayotayarishwa baada ya kila miaka miwili imesema kuwa janga la virusi vya corona limeongeza hali ya kutokuwa na usawa kote ulimwenguni kwani maskini waliathirika zaidi kutokana na ugonjwa huo na athari zake za kiuchumi.

Ripoti hiyo imeendelea kusema kwamba utafiti wake wa CRI unaonesha wazi kwamba serikali nyingi duniani zilishindwa kuthibiti ongezeko hilo la hatari la ukosefu wa usawa.

Oxfam pia ilitathmini serikali 161 kutoka mwaka 2020 hadi 2022, baada ya kile kilichoitwa "dharura kubwa zaidi ya afya duniani katika karne moja". Nusu ya mataifa yaliyohusika yalipunguza matumizi yao ya ulinzi wa kijamii na asilimia 70 yalipunguza matumizi katika sekta ya elimu.

Brasilien I Sao Paulo I Jardim Angela
Hali ya ukosefu wa usawa wa kijamii inaonekana dhahiri shahiri katika wilaya hii ya Jardim Angela mjini Sao Paulo, Brazil, ambapo majumba ya kifahari yanatazamana na karibu la eneo la msongamano linalokaliwa na watu maskini.Picha: Christian Franz Tragni/Imago

Soma pia: Ripoti: Shirika la Oxfam lasema njaa inayochochewa na hali mbaya ya hewa yaongezeka zaidi ya maradufu katika nchi zilizoathirika.

Janga hilo lilipunguza matumizi ya watumiaji kutokana na vizuizi vya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona na badala yake kusababisha kupungua kwa mapato ya ushuru. Hata hivyo mataifa 143 kati ya 161 yalishindwa kuongeza ushuru kwa matajiri na mataifa 11 yalichagua kupunguza ushuru wao.

Kundi dogo la serikali laaibisha serikali nyingine

Utafiti huo umeongeza kuwa kundi dogo la serikali lilipinga hali hii na kuchukuwa hatua wazi za kupambana na ukosefu wa usawa na kuongeza kuwa mataifa haya yaliaibisha mataifa yaliosalia.

Shirika la Oxfam pia lilifichua kuwa thuluthi mbili za mataifa yalishindwa kuongeza kima cha chini cha mshahara wao kulingana na pato la taifa na kuyaorodhesha kutokana na hatua zao na sera katika sekta tatu ambazo ni, matumizi ya kijamii, kodi, na kazi.

Soma pia:Oxfam: Mabilionea watajirika maradufu wakati wa Covid-19 

Norway iliongoza katika orodha hiyo kama taifa linalofanya vyema zaidi linapokuja suala la kukabiliana na ukosefu wa usawa. Kisha ikafuatwa na Ujerumani, Australia, Belgium na Canada. Ufaransa iliorodheshwa ya 12 huku Uingereza ikiorodheshwa katika nafasi ya 14.

Oxfam yavumbua mifereji ya aina mpya ya kuosha mikono

Umoja wa Mataifa walalamika kuhusu usambazaji usio  sawa wa chanjo

Awali, Umoja wa Mataifana wanaharakati hao walilalamika kuhusu usambazaji usio sawa wa chanjo kutoka mataifa tajiri ya Magharibi kuelekea katika mataifa maskini hasa barani Afrika na kuhatarisha maisha.

Oxfam iliyashtumu mataifa kadhaa na kusema kuwa janga hilo lilipaswa kuwa mwamko wa kushughulikia umaskini kwa ujumla. Oxfam pia ilitoa wito kwa serikali kote duniani zinazofadhiliwa kujiepusha na hatua za kubana matumizi ambazo zingezidisha hali ya maskini. 

Soma pia: Ripoti ya Oxfam: Wanawake hufanya kazi bure wakati mabilionea wakiongeza utajiri

Shirika hilo limeongeza kuwa serikali kote duniani, zinazosaidiwa na taasisi za fedha za kimataifa na ufadhili wa kimataifa, zinahitaji kutekeleza sera ambazo zitapunguza ukosefu wa usawa na kulinda mapato ya watu maskini kutokana na mdororo wa kiuchumi na mfumuko wa bei.