Wanawake hufanya kazi bila malipo, matajiri wafaidika
20 Januari 2020Wakati idadi ya mabilionea imeongezeka mara mbili na kufikia 2,153 katika mwongo uliopita wanawake wameendelea kuwa watu wa chini kimapato katika mfumo wa dunia usiokuwa na haki.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Oxfam iliyochapishwa siku moja kabla ya kongamano la kiuchumi la Davos kuanza, Mabilionea hao wana utajiri mkubwa zaidi kuliko watu bilioni 4.6 ambao ni asilimia 60 ya binadamu wote duniani. Viongozi, wataalamu na wafanyabiashara wanakutana kwenye kongamano hilo linalofanyika katika mji wa Davos, nchini Uswisi kujadili masuala ya dunia.
Ripoti ya shirika hilo la misaada pia inabainisha kwamba wanawake duniani kote kwa pamoja wanafanya kazi kwa muda wa saa bilioni 12 na nusu kila siku bila ya malipo au kutambuliwa kwa namna yoyote licha ya kazi za wanawake hao kuongeza thamani ya dola trilioni 10.8 katika uchumi wa dunia kila mwaka. Kiwango hicho ni mara tatu ya mchango unaotolewa na sekta ya tekinolojia.
Akifafanua juu ya hali hiyo Mkurugenzi wa shirika la Oxfam kanda ya India, Amitabh Behar ameeleza kuwa mfumo wa ugawanaji wa utajiri ni tatizo linalosababisha ongezeko la umasikini duniani kote.
Mkurugenzi huyo amezikosoa serikali za dunia kwa kuwa sehemu ya tatizo kwa kuwaruhusu matajiri waendelee kulimbikiza utajiri mkubwa aghalabu kwa kuwakandamiza wananchi wa kawaida ambapo wengi ni wanawake. Bwana Behar amesema inapasa wanasiasa watunge sheria zitakazohakikisha kwamba matajiri wanatozwa kodi kwa njia inayostahili. Mkurugenzi huyo amezitaka serikali duniani zihakikishe kwamba kodi hizo zinatumika kwa ajili kugharamia huduma za maji, afya na elimu.
Kongamano la uchumi wa dunia ambalo linaadhimisha mwaka wa 50 tangu kuanzishwa, sasa linapasa lizingatie zaidi katika kufanya kazi ya maana badala ya kuwa ni kongamano la mkusanyiko wa tafrija kwa mujibu wa ripoti hiyo ya shirika la Oxfam.
Safari hii kwenye kongamalo hilo mkazo utawekwa pia katika suala la ulinzi wa mazingira sambamba na katika masuala ya kibiashara. Washiriki watakuwa pamoja na mwanaharakati mashuhuri wa mazingira Greta Thunberg na Micah White aliyekuwa mwanzilishi wa kampeni ya kuwapinga matajiri wa taasisi ya fedha ya Wall Street. Wakurugenzi, watu wengine mashuhuri, wanasiasa na rais wa Marekani Donald Trump pia watashiriki kwenye kongamano hilo la mjini Davos.
Vyanzo:/ AFP/RTRE/dw.com/a-52045840