1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

OSLO: Mazungumzo kuhusu mazingira yakwama

2 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCN7

Mazungumzo ya Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira yanayoendelea mjini Oslo nchini Norway yamekwama licha ya hofu ya ongezeko la joto la duniani.

Viongozi wa serikali mbalimbali hawajafaulu kupiga hatua katika juhudi za kurefusha mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na ongezeko la joto duniani.

Hapo awali katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amesema mabadiliko ya hali ya hewa yanasababisha hatari kubwa kwa ulimwengu kama vita.

Akiwahutubia wanafunzi katika baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Ban Ki Moon ameitolea mwito Marekani iongoze juhudi za kukabiliana na ongezeko la joto duniani.

´Natumai kwamba Marekani kama ilivyoongoza katika uvumbuzi wa teknolojia, itaongoza pia katika maswala haya muhimu na ya dharura kwa maendeleo ya pamoja ya binadamu.´

Ban Ki Moon amesema ipo haja ya kuunda mkakati madhubuti wa kukabiliana na maswala ya kimazingira.

Mwezi uliopita jopo la wanasayansi wa mazingira liliwasilisha ripoti iliyooonya juu ya ukame, kuongezeka kwa kima cha maji baharini na joto kali. Ripoti hiyo pia ilimlaumu binadamu kwa kusababisha ongezeko la joto duniani.