1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Omar al-Bashir akiri kupokea mamilioni kinyume na sheria

Daniel Gakuba
31 Agosti 2019

Aliyekuwa rais wa Sudan Omar al-Bashir amekiri mahakamani kuwa alipokea mamilioni ya dola za kimarekani kutoka familia ya kifalme ya Saudi Arabia kwa njia zisizo halali. Akikutwa na hatia anaweza kufungwa miaka 10 jela.

https://p.dw.com/p/3Onhl
Sudan Khartum | Ex-Präsident Umar al-Baschir vor Gericht
Rais wa zamani wa Sudan Omar al-Bashir kizimbaniPicha: Getty Images/AFP/E. Hamid

Mahakama nchini Sudan imemfungulia rais wa zamani wa nchi hiyo Omar al-Bashir mashtaka rasmi ya rushwa na kupokea fedha kutoka nje ya nchi kwa njia zilizo kinyume na sheria.

Akizungumza katika kikao cha tatu cha mahakama inayosikiliza kesi ya Bashiri, Jaji Al-Sadiq Abdelrahman amesema fedha za kigeni za mataifa mbali mbali zilikutwa nyumbani kwa Omar al-Bashir baada ya utawala wake kuangushwa. Amesema maafisa wa utawala walikamata euro milioni 6.9, dola za kimarekani zaidi ya laki 3.5 na pauni za Sudan milioni 5.7 zote katika pesa taslimu zilizopatikana kwa njia zisizo halali.

Mamilioni yaliyosafirishwa kwa ndege binafsi

Alipoulizwa alikozipata fedha hizo, Bashiri amekiri kuwa alizipokea kutoka kwa watu walio katika familia ya kifalme ya Saudi Arabia.

Sudans neuer Premierminister Abdalla Hamdok
Waziri Mkuu mpya wa Sudan Abdalla HamdokPicha: picture-alliance/AP Photo

''Meneja wa ofisi yangu alipokea simu kutoka ofisi ya Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman, ambapo aliarifiwa kuwa walikuwa wametuma ujumbe ambao ungewasili Sudan kwa ndege binafsi.'' Bashir ameiambia mahakama wakati wa kusikilizwa kesi dhidi yake, na kuongeza kuwa mrithi huyo wa Ufalme wa Saudi Arabia hakutaka jina lake lionekane katika nyaraka za kuzipokea fedha hizo.

Soma zaidi: Sudan: Jeshi lashindwa kuwaondoa waandamanaji 

Bashir amesema hiyo ndio sababu ya kuzitunza fedha hizo nyumbani kwake, kwa sababu iwapo zingepelekwa katika Benki Kuu ya Sudan, au katika wizara ya fedha ya nchi hiyo, ingekuwa lazima kueleza zilikotoka.

Uwezekano wa kifungo cha miaka mingi gerezani

Jaji amesema kujipatia mali kwa njia haramu ni kosa linaloadhibiwa kwa kifungo cha hadi miaka 10 jela, na matumizi ya fedha za kigeni kinyume cha sheria huadhibiwa kwa kifungo cha miaka mitatu gerezani.

BG Frauen im Sudan
Vuguvugu la maandamano ya umma lilimaliza utawala wa miongo mitatu ya Omar al-BashirPicha: Getty Images/AFP/E. Hamid

Awali, mwendesha mashtaka alikuwa ameiambia mahakama kwamba Bashir alipokea dola milioni 90 kutoka familia ya kifalme ya Saudi Arabia. Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa kesi dhidi ya kiongozi huyo wa zamanai wa Sudan imeahirishwa hadi tarehe 7 mwezi ujao wa Septemba.

Omar al-Bashir aliondolewa madarakani Aprili mwaka huu baada ya maandamano makubwa ya umma dhidi ya utawala wake wa miongo mitatu. Bashiri anatafutwa pia na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC yenye makao yake mjini the Hague, kwa tuhuma za kuhusika katika mauaji ya halaiki katika jimbo la Darfur Magharibi mwa Sudan.

Soma zaidi: HRW lataka uchunguzi ufanyike Sudan

Mwendeshamashtaka mkuu wa mahakama hiyo Fatou Bensouda amewatolewa wito watu wa Sudan kuunga mkono mkondo wa sheria kwa kumkabidhi Bashir katika mahakama ya ICC ili akawajibishwe kwa uhalifu anaotuhumiwa kuufanya. Nchini Sudan kwenyewe, waendeshamashtaka wamesema Omar al-Bashir atashitakiwa kuamuru mauaji dhidi ya waandamanaji walioshiriki katika vuguvugu lililomng'oa madarakani.

Hivi sasa Sudan iko katika mchakato wa kuelekea kwenye serikali ya kiraia, kufuatia muafaka uliopatikana kati ya viongozi wa waandamanaji na majenerali wa jeshi waliompindua Bashir.

afpe, dpae