1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Changamoto kwa watoto wa wahamiaji Ulaya

29 Mei 2018

Utafiti uliyofanywa na Shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo barani Ulaya OECD umegundua watoto waliyo na wazazi waliyohamia Ulaya wanapitia changamoto linapokuja suala la elimu na nafasi za jira barani humo.

https://p.dw.com/p/2yVHN
Deutschland Frau Muslimische Frau holt Kinder von Schule ab
Picha: picture-alliance/W. Rothermel

Shirika hilo la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo barani Ulaya OECD lililo na makao yake mjini Paris Ufaransa, limesema watoto waliyozaliwa barani Ulaya kwa wazazi wasiotoka katika bara hilo wanaendelea kupata changamoto chungu nzima katika masuala ya elimu na soko la ajira.

Symbolbild | Schule Unterricht Schulklasse Schüler
Badhi ya wanafunzi wakiwa darasani nchini UjerumaniPicha: imago/O. Ring

Utafiti uliyofanywa na shirika hilo umegundua kuwa watoto wa wahamiaji katika bara zima la Ulaya, waliyowasili baada ya vita vya pili vya dunia wanaojulikana kama "wafanyakazi wageni” wana nafasi finyu katika safari yao ya kumaliza shule ya sekondari au kupata nafasi ya ajira kuliko watoto waliyo na wazazi waliyozaliwa Ulaya.

Hata hivyo utafiti huo pia umegundua kwamba nafasi zilizopo kwa sasa kwa watoto wa wahamiaji ni nzuri kuliko hali ilivyokuwa kwa wazazi wao miaka ya nyuma, hii inaonesha kuwa maisha ya kijamii na kiuchumi ya watoto hao ni tofauti kuliko ya watoto wengine.

Kizazi cha kwanza cha wahamiaji hawana vyeti rasmi vya kumaliza sekondari.

Hali hii imeonekana wazi nchini Ujerumani. Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 50 ya wanawake na asilimia 30 ya wanaume ambao ni kizazi cha kwanza cha wahamiaji kutoka Uturuki na iliyokuwa Yugoslavia ya zamani hawakuwa na vyeti rasmi vya kumaliza masomo ya sekondari, lakini mwaka 2012 zaidi ya asilimia 90 ya watoto wa wahamiaji waliyozaliwa nchini Ujerumani walikamilisha masomo yao.

Muslimische Frauen mit Kindern
Baadhi ya wahamiaji wakiwa mjini Berlin UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa/W.Rothermel

Aidha robo moja  ya watoto waliyo na wazazi kutoka Yugoslavia walipata kile kinachojulikana kama "Abitur" — Ujuzi au sifa inayotolewa katika shule za maandalizi ya ujuzi Fulani nchini Ujerumani.  Kwa kulinganisha nusu ya wanafunzi wote nchini Ujerumani wamehitimu kwa cheti cha kidato cha sita "Abitur."

Aidha idadi ya wanafunzi wanaotafuta elimu ya juu bado ni ndogo mno ukilinganisha na watoto wanaozaliwa na wazazi wanaotoka Ulaya, ukizingatia  nafasi za kuvutia zinazotolewa na  shule za mafunzo ya kazi.

OECD iliyoanzishwa mwaka 1961 ni Shirika la kiuchumi la serikali likiwa na nchi 35 wanachama . Kazi yake ni kukuza sera za kuimarisha maisha ya watu kuchumi na kijamii duniani kote.

Mwandishi Amina Abubakar/DW Page

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman