1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama, Rais wa kwanza wa Marekani kuizuru Ethiopia

27 Julai 2015

Rais wa Marekani Barack Obama ameanza ziara ya siku mbili nchini Ethiopia, akiwa Rais wa Kwanza wa Marekani kuzuru taifa hilo la pili barani Afrika lenye idadi kubwa ya watu na ndipo yalipo makao makuu ya Umoja wa Afrika

https://p.dw.com/p/1G532
Picha: Reuters/J. Ernst

Rais Obama akitokea Kenya alikokuwa kwa ziara ya siku tatu na alikoendesha mkutano wa kimtaifa wa wajasiriamali, amewasili katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa jana jioni na kulakiwa na mwenyeji wake waziri mkuu wa Ethiopia Haile Mariam Desalegn

Rais huyo wa Marekani anatarajiwa kufanya mazungumzo na serikali ya Ethiopia ambayo ni mshirika muhimu lakini inayoshutumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu na ukandamizaji wa demokrasia.

Sudan Kusini iko katika ajenda

Obama anatarajiwa pia kufanya mazungumzo na viongozi wa kanda hiyo kuhusu vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan Kusini katika juhudi za kuchukua hatua madhubuti dhidi ya viongozi wa Sudan Kusini iwapo watashindwa kuvimaliza vita hivyo ifikapo kati kati ya mwezi ujao.

Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn akimkaribisha Rais wa Marekani Barack Obama mjini Addis Ababa
Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn akimkaribisha Rais wa Marekani Barack Obama mjini Addis AbabaPicha: Reuters/T. Negeri

Hapo Kesho, Obama atakuwa Rais wa kwanza wa Marekani kuhutubia katika umoja wa Afrika wenye nchi wanachama 54. Rais wa Halmashauri ya umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini Zuma ameisifu ziara hiyo aliyoitaja kuwa ya kihistoria na hatua madhubuti kuelekea kutanua na kuboresha uhusiano kati ya Umoja huo na Marekani.

Ethiopia kama Kenya, imekuwa katika mstari wa mbele katika vita dhidi ya waasi wa Al Shabab nchini Somalia. Nchi hizo mbili zina majeshi nchini Somalia kama sehemu ya ujumbe wa kijeshi wa Umoja wa Afrika unaoungwa mkono na Marekani. Suala la usalama linatarajiwa kuwa mojawapo ya ajenda kuu ya mazungumzo kati ya Obama na mwenyeji wake.

Demokrasia na haki za binadamu Ethiopia kumulikwa

Ziara ya Obama nchini Ethiopia inakuja miezi miwili baada ya chaguzi nchini humo ambazo chama tawala kinachoongozwa na Haile Mariam Desalegn kilishinda viti vyote 546 vya bunge. Vyama vya upinzani vimelalamika kukandamizwa na serikali na kudai serikali ilitumia mbinu za kiimla kushinda katika uchaguzi huo.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema inatambua kuwepo vizuizi vya uhuru wa kujieleza, kuwepo kesi zinazochochewa kisiasa na kuteswa na kukandamizwa kwa wanasiasa wa upinzani na wanahabari Ethiopia.

Masuala hayo ya demokrasia yanatarajiwa kuangaziwa katika ziara hiyo ya kiongozi wa Marekani nchini Ethiopia ikizingatiwa alizungumzia wazi masuala ya haki za binadamu na ufisadi nchini Kenya mwishoni mwa juma. Obama pia atafanya mazungumzo na viongozi wa mashirika ya kiraia.

Licha ya rekodi mbaya ya haki za binadamu na kutokuwepo kwa uhuru wa kidemokrasia, Ethiopia imepiga hatua za kipigiwa mfano kutoka kuwa taifa maskini lililojulikana duniani kwa baa la njaa lililoikumba mwaka 1984 na kukua kiuchumi, kuimarika pakubwa katika miundo mbinu na kuwa mojawapo ya nchi za Afrika zinazovutia wawekezaji.

Mwandishi:Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Gakuba Daniel