Obama aitaka Kenya kufuata barabara ya maendeleo
27 Julai 2015Ndege iliyombeba Rais Barrack Obama iliondoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta saa kumi na dakika 20 kueleka mjini Addis Ababa, Ethiopia. Rais Obama amekamilisha ziara yake nchini Kenya kwa kukutana na waakilishi wa mashirika ya kijamii ambapo alizungumzia hasa swala la ugaidi na jinsi ya kukabiliana na janga hilo.
“Hapa Kenya ugaidi umesababisha vifo vya watu wengi sana. Tunakumbuka Wakenya na Wamarekani waliofariki katika shambulizi la bomu katika ubalozi wetu miaka ya tisini. Tunakumbuka wakenya wasio na hatia waliouawa katika jumba la kibiashara la westgate. Tulitoa machozi wakati wanafunzi wapatao 150 waliouwawa huko Garissa”
Kwenye hotuba yake kwa taifa awali katika uwanja wa michezo wa Safaricom huko Kasarani, Rais Obama amezungumzia maswala kadhaa muhimu ikiwa ni pamoja na ufisadi, ubaguzi wa kijinsia na ushirikishi wa vijana katika maswala ya maendeleo.
Kuhusu Ugaidi Rais Obama amesema atashirikiana na Kenya kupambana na janga hilo.
Rais Obama ameelekea mjini Addis Ababa Ethiopia kuhudhuria kongamano la viongozi wa mataifa ya Umoja wa Afrika ambapo atashiriki kwenye mazungumzo kuhusu mzozo wa Sudan.
Rais Obama aliyekuwa nchini Kenya tangu siku ya Ijumaa jioni, hapo jana akiwa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta walifungua rasmi Kongamano la sita la ulimwengu kuhusu ujasiriamali lililohudhuriwa na wajumbe wapatao 4,000 wakiwemo wajasiriamali mashuhuri zaidi ya 200 kutoka Marekani.
Obaba na mwenyeji wake Uhuru Kenyatta vilevile walifanya mashauri katika ikulu ya Nairobi, mashauri yaliyozingatia uhusiano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili, ushirikiano katika maswala ya usalama na mswala ya kiijamii.
“Marekani ni nchi ya wajasiriamali.Ina uwezo wa kujenga misingi ya biashara mpya na ninatumaini wajasiriamali hawa watachukua fursa iliyopo ya nafasi za uwekezaji tulizonazo hapa Kenya na Afrika kwa ujumla. Ningependa kupongeza uongozi wa Rais Obama kwa kupigania kuongezwa muda mkataba wa AGOA”
Mikataba kadhaa imetiwa saini ikiwemo kuongezwa muda kwa mkataba wa AGOA kwa kipindi cha miaka kumi zaidi na kuongezwa muda kwa visa za wakenya wanaosafiri nchini Marekani hadi miaka mitano.
Marekani tayari imeahidi msaada wa dola milioni 100 kufadhili miradi ya ujasiriamali kwa wanawake barani Afrika ambapo vituo vya ujasiriamali vitajengwa kwanza nchini Kenya, Zambia na Mali. Obama ni rais wa kwanza wa Marekani kuzuru Kenya na Ethiopia akiwa madarakani.
Ziara ya Obama nchini Kenya imekuwa ziara ya kihistoria kwani hakuja Kenya tu kama kiongozi wa taifa lililo na ushawishi mkubwa duniani bali amefika Kenya kama mwana wa Mkenya aliye na mizizi yake nchini Kenya.
Mwandishi: Alfred Kiti/DW Nairobi
Mhariri: Mohamed Dahman