1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama na Cameron lao moja kwa Gaddafi

25 Mei 2011

Rais Barack Obama wa Marekani na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, wamekubaliana kuongeza shinikizo dhidi ya Muammar Gaddafi, lakini wameondosha uwezekano wa kupeleka wanajeshi wa ardhini huko Libya

https://p.dw.com/p/11O1v
Rais Barack Obama (kushoto) na mwenyeji wake, David Cameron
Rais Barack Obama (kushoto) na mwenyeji wake, David CameronPicha: AP

Wakizungumza na waandishi wa habari mchana wa leo jijini London, mara baada ya kukamilisha mazungumzo yao, Rais Obama na Waziri Mkuu Cameron wameonesha kukubaliana kwenye mambo mengi ya msingi kuhusiana na siasa za nje za mataifa yao.

Mgogoro wa sasa Libya umeonekana kuchukuwa sehemu kubwa ya mazungumzo hayo, ambapo viongozi hao wameonesha kuridhika kwao na hatua zilizopigwa katika operesheni ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO nchini humo.

Hata hivyo, wote wawili wameelezea haja ya kuwepo subira wakati operesheni hii ikiendelea na huku kutaka pia kuwepo kwa kasi zaidi katika kile walichokiita "utekelezaji wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwalinda raia dhidi ya mashambulizi ya vikosi vya Kanali Gaddafi".

"Mimi na Rais Obama tunakubaliana kwamba suala la kubadilisha utawala halimo kwenye azimio la baraza la usalama la umoja wa mataifa. Azimio hilo linahusu kuwalinda raia dhidi ya mashambulizi yoyote na kuchukua hatua zote zinazolazimu kutekeleza hilo. Lakini viongozi wa kisiasa, tukiwemo sisi, tunajiuliza inawezekanaje kuwalinda raia wakati Gaddafi bado yuko madarakani. Ndio maana tukawa tunasisitiza haja ya Gaddafi kuondoka madarakani na kuondoka Libya." Amesema Cameron.

Muammar Gaddafi
Muammar GaddafiPicha: dapd

Hata hivyo, Rais Obama amesema kwamba suala la kummaliza nguvu Kanali Gaddafi ni mchakato unaokwenda taratibu na, hivyo, ni jambo la lazima kuwasaidia wapinzani kujiimarisha wenyewe. Katika hili viongozi wote wawili wamekubaliana haja ya kuongeza kiwango kikubwa cha "rasilimali" kwenye operesheni hii ya Libya.

Lakini suala kubwa kwa Rais Obama lilikuwa ni lile la suluhu ya mgogoro wa Mashariki ya Kati, ambapo amerejelea msimamo wa serikali yake wa kuwepo kwa mataifa mawili huru ya Israel na Palestina. Hata hivyo, akasisitiza upinzani wake kwa azma ya Wapalestina kulipeleka suala hili kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hapo mwezi Septemba.

"Naamini kwa dhati kabisa kwamba, kwa Wapalestina kutumia njia ya Umoja wa Mataifa badala ya kukaa pamoja na Waisraili ni kosa." Amesema Rais Obama.

Kuhusiana na hali inavyoendelea sasa nchini Yemen, Rais Obama amemtaka Rais Ali Abdullah Saleh kutekeleza haraka ahadi yake ya kuwachia madaraka kwa msaidizi wake, katika wakati huu ambao taifa hilo la Ghuba likiselelea kwenye umwagikaji damu.

Obama na Cameron wamekubaliana kwamba watawashinikiza viongozi wenzao wa mataifa manane tajiri duniani, G8, kuwa na mpango maalum wa kuzisaidia kiuchumi na kisiasa zile nchi za Kiarabu zinazopigania mabadiliko hivi sasa.

"Mimi na Rais Obama tumekubaliana kusimama na wale wanaopigania uhuru. Na ujumbe huu ndio tutakaokwenda nao kesho kwenye mkutano wa G8." Amesema Cameron.

Viongozi hao wawili wanatarajiwa kujiunga na wenzao wa G8 katika mkutano unaoanza kesho kwenye mji wa Deauville, nchini Ufaransa.

Baadaye jioni ya leo, Rais Obama amewahutubia wabunge wa mabunge yote mawili ya Uingereza.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPAE/AFPE
Mhariri: Othman Miraji