Netanyahu akataa pendekezo la Obama
21 Mei 2011Kufuatia mazungumzo hayo, Obama alikiri kuwa kulikuwepo tofauti za maoni kuhusu njia ya kupata amani katika kanda hiyo na akaongezea kuwa kwa Marekani, usalama wa Israel ni suala lenye umuhimu mkubwa.
Mkutano wa viongozi huo umefanyika kufuatia mivutano iliyozuka baada ya Obama hivi karibuni kupendekeza kuwa taifa la Palestina litakaloundwa siku zijazo,liwe chini ya msingi wa mipaka iliyokuwepo kabla ya mwaka 1967. Netanyahu amepinga vikali pendekezo hilo. Amesema, anaamini kuwa Wapalestina watapaswa kukubali baadhi ya mambo yaliyokuwa hali halisi ya kimsingi. Israel ipo tayari kuafikiana ili kupata amani lakini haiwezi kurejea katika mipaka ya mwaka 1967, kwani mipaka hiyo haiwezi kulindwa. Vile vile mipaka hiyo haizingatii abadiliko ya kijamii yaliyotokea katika kipindi cha miaka 44 iliyopita. Hata hivyo, Netanyahu amesema kuwa ataendelea kushirikiana na Obama kutafuta ufumbuzi wa amani utakaohakikisha usalama wa Israel.